Zimbabwe yapiga kura huku Mnangagwa akitarajiwa kushinda
23 Agosti 2023Matukio ya kucheleweshwa upigaji kura yameukumba uchaguzi mkuu wa Zmbabwe leo wakati Emmerson Mnangagwa akitafuta kuongoza kwa muhula wa pili na wa mwisho.
Tume ya uchaguzi ya Zimbabwe ilikiri kucheleweshwa usambazaji wa karatasi za kura katika baadhi ya vituo vya kupigia kura na kusema hali hiyo ilisababishwa na kuchelewa kuchapishwa karatasi hizo kutokana na kesi nyingi zilizowasilishwa mahakamani.Rais Mnangagwa ataweza kurejea madarakani?
Huu ni uchaguzi mkuu wa pili tangu kuondolewa kupitia mapinduzi ya 2017 aliyekuwa kiongozi wa muda mrefu aliyetawala kimabavu Robert Mugabe.
Wagombea 12 wa urais wanashiriki, lakini mpambano mkali unatarajiwa kuwa kati ya Mnangagwa mwenye umri wa miaka 80, anayefahamika kama "mamba" na kiongozi wa upinzani mwenye umri wa miaka 45 Nelson Chamisa.Nelson Chamisa, kijana anayepambana na Mnangagwa
Baada ya kupiga kura yake, Mnangagwa alielezea matumaini kuwa atashinda na kuwahimiza watu kudumisha amani. Mnangagwa alimpiku kwa kura chache Chamisa katika uchaguzi uliokumbwa na utata wa mwaka wa 2018. Chamisa anatumai kuvunja udhibiti wa chama tawala ZANU-PF kilichoshikilia madaraka kwa miaka 43.