1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zimbabwe yasubiri matokeo ya uchaguzi

2 Agosti 2018

Hali ya utulivu inashuhudiwa Zimbabwe wakati ikisubiri kwa shauku kubwa matokeo ya uchaguzi wa kihistoria wa rais baada ya wanajeshi hapo jana kuwafyatulia risasi waandamanaji waliokuwa wakipinga madai ya wizi wa kura

https://p.dw.com/p/32USe
Zimbabwe, Wasserwerfer
Picha: picture-alliance/T.Mukwazhi

Rais Emmerson Mnangagwa ametoa wito wa kufanyika uchunguzi huru kuhusiana na vurugu za jana akisema kuwa waliohusika wanapaswa kukamatwa na kushitakiwa. Aidha amesema kuwa amezungumza na kiongozi wa upinzani Nelson Chamisa katika juhudi za kutuliza hali na kuumaliza kwa amani mzozo huo wa uchaguzi. Serikali iliapa jana usiku kuimarisha hatua za usalama ili kuzuia vurugu zaidi baada ya jeshi kutumia risasi za moto kuwatawanya waandamanaji wa chama cha upinzani cha Movement for Democratic Change – MDC katika mji mkuu Harare, na kusababisha vifo vya watu watatu.

Katika kikao cha waandishi wa habari, Waziri wa Mambo ya Ndani Obert Mpofu alionya kuwa serikali haitavumilia aina yoyote ya vitendo vya vurugu vilivyoshuhudiwa jana. Wanajeshi wameweka doria katika mitaa ya mji mkuu Harare ambayo inashuhudia utulivu baada ya makabiliano ya jana. Tovuti ya tume ya uchaguzi, ambayo inatarajiwa kuanza kutangaza matokeo ya urais leo, ilishambuliwa na wadukuzi wasiojulikana usiku wa kuamkia leo.

Simbabwe, Harare: Anhänger der Opposition Chamisas MDC-Partei protestieren auf der Straße
Wapinzani wanadai kulikuwa na wizi wa kuraPicha: Reuters/S. Sibeko

Wafuasi wa MDC wanadai kiongozi wao Nelson Chamisa aliye na umri wa miaka 40, alishinda uchaguzi wa rais. Kimesema jeshi lilifyatua risasi bila sababu yoyote na kusababisha vifo vya raia wasiokuwa na silaha. Nkululeko Sibanda ni msemaji wa MDC "Raia wanaruhusiwa kudai heshima ya haki zao kwa njia ya halali. Vurugu zozote zinapaswa kukabiliwa na polisi ambao wana mafunzo ya kuweka utulivu. Wanajeshi wamepewa mafunzo ya kuuwa wakati wa vita. Kwani tuko vitani? Je, raia ni maadui wa serikali? Kupoteza maisha ndicho kitu kinachotuumiza sana"

Timu ya uangalizi ya Jumuiya ya Madola imeiomba tume ya uchaguzi kutangaza haraka matokeo ya urais ikiongeza kuwa jeshi lilitumia nguvu kupita kiasi katika kukabiliana na waandamanaji. John Dramani Mahama ni kiongozi wa timu ya Jumuiya ya Madola "Tunaamini kuwa kama tume ya uchaguzi itaharakisha utoaji matokeo, basi inakuwa rahisi kwa kila chama katika mchakato huo kuidhinisha kama matokeo hayo ni halali au la. Na ndio maana kucheleweshwa matokeo hayo kunasababisha wasiwasi"

Waangalizi wa Umoja wa Ulaya awali walisema mchakato wa uchaguzi haukutoa mazingira sawa kwa washiriki na ukakosa uaminifu. Uingereza ilitoa wito wa utulivu na kujizuia, na kuwataka viongozi kuwajibika katika wakati huu muhimu. Matokeo rasmi ya mwanzo yalionyesha jana kuwa chama tawala cha ZANU-PF kilishinda viti vingi vya bunge – na hivyo kuongeza matumaini ya Rais Emmerson Mnangagwa mwenye umri wa miaka 75, kuendelea kutawala. Tume ya uchaguzi ilisema jana kuwa kati ya viti 210 vya bunge, 205 vimehesabiwa ambapo ZANU PF ina viti 144 na Muungano wa MDC ukiwa na viti 61.

Matokeo ya awali ya kinyang'anyiro cha urais yalitarajiwa kutolewa jana lakini hilo halikufanyika. Tume ya uchaguzi ilionya kuwa matokeo ya mwisho ya duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais yatajulikana Ijumaa au Jumamosi.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Iddi Ssessanga