1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zoezi la kuhesabu kura laanza Uganda

14 Januari 2021

Zoezi la kuhesabu kura limeanza nchini Uganda baada ya vituo vya kupigia kura kufungwa katika uchaguzi wa rais na bunge uliofanyika leo. Raia wa Uganda wamejitokeza kwa wingi kushiriki zoezi hilo.

https://p.dw.com/p/3nuto
Afrika Uganda Wahlen
Picha: Jerome Delay/AP/picture alliance

Polisi na wanajeshi walionekana kulinda doria katika mitaa ya jiji kuu la Kampala. Uchaguzi wa leo umemweka katika ushindani mkubwa rais wa muda mrefu Yoweri Museveni na mwanamuziki aliyegeuka kuwa mwanasiasa Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine. Zoezi hilo limefanyika wakati serikali ikizima huduma ya intaneti na mitandao ya kijamii katika taifa hilo lenye wakaazi takribani milioni 46.  

Shughuli ya kupiga kura ilianza kwa kuchelewa kwa muda wa takriban saa moja hadi saa moja na nusu katika vituo sita vya kupiga kura huku karatasi za kupiga kura zikicheleweshwa. Msemaji wa chama tawala amesema kuwa shughuli ya kupiga kura ilianza kuchelewa katika baadhi ya maeneo kutokana na hitilafu kwenye vifaa vya kielektoniki vya kupigia kura.

Serikali mnamo siku ya Jumatano iliagiza kukatizwa kwa huduma za intaneti kwa muda usiojulikana hiyo ikiwa ni siku moja baada ya kuifungia mitandao yote ya kijamii.

soma zaidi: Ni Museveni au Bobi Wine Uganda?

Msanii wa nyimbo za mtindo wa Reggae Bobi Wine mwenye umri wa miaka 38 anawakilisha vijana wengi nchini humo wanaosema kuwa rais Museven aliye na umri wa miaka 76 ni dikteta ambaye ameshindwa kushughulikia matatizo ya ukosefu ajira, ufisadi na kuongezeka kwa deni la taifa.

‘Wamechoshwa na MuseveniI'

Uganda Wahlen l Zerrissenes Wahlplakat von Präsident Museveni
Rais wa Uganda Yoweri MuseveniPicha: Baz Ratner/REUTERS

Museveni ambaye amekuwa uongozini tangu mwaka 1986, amesema kijana Bobi Wine mwanagenzi katika mambo ya siasa anaungwa mkono na serikali za nje pamoja na watu wanaounga mkono mahusiano ya jinsia moja tofauti na uongozi wake utawala wake unatoa uhakika wa  utulivu, maendeleo, ikiwa ni pamoja na mabwawa barabara umeme wa maji.

Idadi ya wapiga kura waliojisajili ni milioni 17.7. Rogers Mulindwa, msemaji wa chama tawala cha NRC amesema raia wengi wa Uganda wamejitokeza kwa wingi kupiga kura. Matokeo ya kwanza yanatarajiwa kutolewa mnamo siku ya Jumamosi jioni

Gari lililombeba Bobi Wine lilipowasili katika kituo cha kupiga kura lilizungukwa na polisi huku wafuasi wake wakiimba na kushangilia. Baadhi ya raia waliokuwa wakisubiri kupiga kura zao, walisema kuwa walikuwa wanaogopa maafisa wa usalama lakini wamejitolea kumpigia kura Wine.

Sababu zilizotolewa na serikali za kuzuia mikutano

Kumekuwa na ghasia zaidi wakati wa kampeini katika uchaguzi wa mwaka huu ikilinganishwa na chaguzi zilizopita. Watu kadhaa wameuawa wakati wa makabiliano na wafuasi wa Bobi Wine kwenye mikutano yake . Wagombea wa upinzani, wafuasi na wasimamizi wa kampeini za uchaguzi wa upande wa upinzani wamekuwa wakikamatwa mara kwa mara.

Serikali imesema inazuia mikusanyiko isiyostahili kwa ajili ya kuzuia kuongezeka kwa maambukizi ya virusi vya corona. Upinzani nao unasema marufuku dhidi ya mikutano yao katika baadhi ya maeneo nchini Uganda ni njia iliyotumiwa kuwakandamiza.

soma zaidi: Raia wa Uganda kuchagua Rais na Bunge jipya

Muhamad Barugahare, mwendeshaji boda boda wa umri wa miaka 31, anasema kuwa Museveni ndiye mtu wa pekee anayeweza kuhakikisha amani nchini humo na kwamba hawataki kubahatisha na kijana mdogo, akimaanisha Wine.

Maoni tofauti yatolewa kuhusu anayetarajiwa kupata ushindi

Uganda Wahlen l Wahlplakate in Kampala
Picha: Baz Ratner/REUTERS

Wachambuzi wanasema ijapokuwa Wine anapendwa na wafuasi wanaoghadhabishwa na uongozi wa Museveni lakini rais huyo mkongwe bado ana nafasi kubwa ya kushinda.

Mjumbe mmoja wa Umoja wa Ulaya amesema kwa maafisa wa usalama kuwepo barabarani ili kuhakikisha utulivu lakini kuwepo,kwao pia kubaibua hali ya wasiwasi.

Wine, ambaye majina yake rasmi ni Robert Kyagulanyi Ssentamu, amewahimiza wafuasi wake kufuatilia zoezi la kuhesabu kura hesabu na kutuma picha za karatasi za matokeo kupitia kwenye mfumo wa U Vote ingawa kukosekana kwa huduma ya Intaneti kunaweza kutatiza hatua hiyo.

Chanzo: afp,reuters