Afrika 2025: Mapambano ya demokrasia na ukuaji
1 Januari 2025Nchini Msumbiji, wachambuzi wa kisiasa wana hofu kuwa machafuko yaliyofuatia uchaguzi wa Rais wa Oktoba 2024 yataendelea hata baada ya mwaka mpya. Uchaguzi huo ulisababisha maandamano ya vurugu, ambapo wafuasi wa kiongozi wa upinzani Venâncio Mondlane walikishutumu chama tawala cha FRELIMO kwa uchakachuaji wa kura.
PODEMOS, chama cha upinzani kilichomuunga mkono Mondlane, kimewasilisha kesi katika Mahakama ya Katiba na kutaka mazungumzo na FRELIMO, chama kilichotawala tangu uhuru wa nchi hiyo kutoka Ureno karibu nusu karne iliyopita.
Adriano Nuvunga, Mkurugenzi wa Kituo cha Demokrasia na Haki za Binadamu, amesema mazungumzo yanayopendekezwa kuhusu mfumo wa haki wa uchaguzi hayachukuliwi kwa uzito na serikali.
Soma pia: Baraza la katiba laidhinisha matokeo ya uchaguzi Msumbiji
Katika mahojiano na DW, aliielezea hali katika mji mkuu Maputo kuwa karibu na vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Katika mataifa mengine ya Afrika, changamoto za kuheshimu kanuni za kidemokrasia zinaendelea.
Serwah Prempeh kutoka Taasisi ya Utafiti wa Sera za Afrika (APRI) anaonya kuwa, licha ya juhudi za kukuza demokrasia katika nchi kama Tunisia na Mauritania, changamoto za uchaguzi zimebaki.
Yeye anasisitiza kuwa mafanikio yanategemea kuimarisha taasisi za kitaifa ili kuboresha uwazi wa uchaguzi na mfumo wa vyama vingi.
Uchaguzi kusini mwa Afrika na shinikizo la mafanikio
Mwaka 2024, uchaguzi umefanyika kwa amani katika nchi kama Mauritius, Botswana, na Senegal ambapo vyama tawala vimebwagwa, huku Afrika Kusini ikishuhudia mabadiliko ya kihistoria kutoka utawala wa chama kimoja hadi serikali ya umoja wa kitaifa.
Soma pia: Serikali ya Botswana yasifiwa kwa kukabidhi madaraka kwa amani
Kwa Afrika Kusini, nchi kubwa ya kiviwanda barani humo, yote yamo kwenye mstari baada ya chama cha upinzani cha Democratic Alliance (DA) kuunda muungano na African National Congress (ANC), kufuatia kushindwa kwa kihistoria kwa ANC katika uchaguzi mkuu: "Serikali ya umoja wa kitaifa iko chini ya shinikizo kutoa matokeo", anasisitiza Silke kwa nia ya uchaguzi wa mitaa mwaka wa 2026.
Ukuaji wa uchumi na uundaji wa ajira ni malengo muhimu kwa serikali mpya ya Afrika Kusini. Marekebisho ya kiuchumi yaliyopendekezwa tayari yameboresha matarajio ya ukuaji, na utabiri wa 2025 ukionyesha ukuaji wa asilimia 1.5 hadi 2.6.
Aidha, Afrika Kusini imechukua nafasi muhimu ya kimataifa kama mwenyekiti wa G20, nchi ya kwanza ya Afrika kushikilia nafasi hiyo. Rais Cyril Ramaphosa anaona nafasi hii kama fursa ya kusukuma ajenda za bara zima, ikiwa ni pamoja na kupambana na umasikini, mabadiliko ya tabianchi, na madeni makubwa.
Ukuaji wa uchumi barani Afrika
Kulingana na Benki ya Dunia, uchumi wa nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara unatarajiwa kukua kwa asilimia 4 ifikapo 2025, ukichochewa na biashara, uwekezaji, na mabadiliko ya kidijitali.
Afrika Mashariki inatarajiwa kuwa eneo linalokua kwa kasi zaidi, na ukuaji wa Pato la Taifa (GDP) unatarajiwa kuongezeka kutoka asilimia 4.9 mwaka 2024 hadi asilimia 5.7 mwaka 2025, kulingana na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).
Soma pia: Viongozi wa Kiafrika watua mjini Beijing kuhudhuria kongamano na China
Hata hivyo, nchi nyingi zinakabiliwa na shinikizo la kifedha kutokana na deni kubwa, usimamizi mbovu wa uchumi, na mfumuko wa bei.
Nchi kama Ghana, Zambia, na Nigeria zinaathiriwa zaidi, huku mikakati ya kuimarisha biashara ndani ya Afrika kupitia Mkataba wa Biashara Huria wa Afrika (AfCFTA) ikionekana kuwa muhimu zaidi.
Migogoro ya kibinadamu na tishio la ugaidi
Licha ya mafanikio ya kiuchumi, migogoro ya kibinadamu na vita bado vinaathiri maendeleo barani Afrika.
Mwisho wa 2024, watu takriban milioni 35 walikuwa wakimbizi wa ndani, wengi wao wakiwa Sudan, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Ethiopia, Nigeria, na Somalia.
Kwa mujibu wa ripoti za ufuatiliaji, idadi hii inaweza kuongezeka ikiwa juhudi za serikali na washirika wake hazitaimarishwa.
Katika kanda za Sahel na Afrika Magharibi, mapinduzi ya kijeshi na serikali za kijeshi zimeendelea kudhoofisha demokrasia, huku ugaidi wa makundi ya itikadi kali za Kiislamu ukisababisha changamoto za usalama.
Gabon imeonyesha matumaini baada ya kupiga hatua kuelekea utawala wa kiraia kufuatia kura ya mabadiliko ya katiba, ingawa uchaguzi wa rais wa Agosti 2025 utakuwa kipimo muhimu cha mafanikio.
Kinyume chake, Cameroon na nchi kama Uganda na Rwanda zimeendelea kuona viongozi wakiongeza muda wao wa mamlaka huku nafasi ya kijamii ikizidi kufungwa.