Afrika katika magazeti ya Ujerumani
24 Novemba 2017Gazeti la Süddeutsche limeandika kwamba chini ya utawala wa Mugabe Mnangagwa alikuwa mkuu wa shirika la ujasusi na pia waziri wa sheria. Watetea haki za binadamu nchini Zimbabwe wanasema Mnangagwa alihusika na mauaji ya maalfu ya watu yaliyofanyika katika jimbo la Matabeleland mnamo miaka ya 80. Gazeti hilo linaeleza kwamba kutokana na unyama alioufanya, watu wa Zimbabwe wamempa Mnangawa jina la mamba. Hatahivyo gazeti hilo la Süddeutsche limemnukuu shujaa huyo wa vita vya ukombozi akisema yuko tayari kuleta mabadiliko ya amani na kuimarisha demokrasia.
Gazeti la Der Spiegel pia limeandika juu ya tufani la kisiasa lililoikumba familia ya Mugabe. Linasema utawala wa Gucci umefikia mwisho baada ya miaka 37 likiwa na maana ya mtindo wa maisha ya mke wa Mugabe, Grace na watoto wake. Lakini kuhusu mabadiliko yaliyotokea mtu hana uhakika iwapo yataleta demokrasia na uhuru nchini Zimbabwe.
Nalo gazeti la Die Welt wiki hii linatanabahisha juu ya njia mpya inayotumiwa sasa na wakimbizi kwenda Ulaya. Njia hiyo ni Morocco na limemnukuu Mkameruni mmoja, Patou Sedrick akisema hajawahi kuona boti nyingi zilizojaa wakimbizi kama anazoziona a sasa nchini Morocco zikianza safari kutokea kila upande. Gazeti la Die Welt linaeleza kuwa kijana huyo mwenyewe aliwahi kuwa mkimbizi na aliyosema yanathibitisha takwimu za shirika la kimataifa la uhamiaji-IOM. Wakimbizi wapatao 18,000 waliwasili nchini Uhispania tangu mwanzoni mwa mwaka huu kwa kutumia mashua.
Kulinganisha na mwaka uliopita idadi hiyo maana yake ni ongezeko la mara tatu. Njia ya hapo awali ambayo ni Libya ilifungwa kuanzia mwezi wa Julai baada ya Italia kuchukua hatua. Serikali ya nchi hiyo ilitoa fedha na misaada mingine yenye thamani ya mamilioni kwa serikali ya Libya na tangu wakati huo hakuna wakimbizi wanaotumia njia hiyo ya Libya. Dunia nzima ilishtushwa na habari juu ya masoko ya watumwa nchini Libya. Watumwa hao wanatoka nchi kadhaa za Afrika.
Katika makala yake wiki hii gazeti la die tageszeitung limeuzingatia mkasa huo na linaeleza kwamba wimbi la ghadhabu lilienea barani Afrika kote baada ya shirika la televisheni la Marekani CNN kuonyesha jinsi waafrika walivyokuwa wanapigwa mnada kwenye masoko nchini Libya kuanzia dola mia nne. Gazeti hilo la die tageszeitung limeeleza kwamba maripota wa CNN walipatiwa ukanda wa video uliokuwa unaonyesha jinsi vijana 12 kutoka Niger walivyokuwa wanauzwa.
Habari hizo zilienea haraka barani Afrika na kuwafanya wasanii mahiri waje juu ikiwa pamoja na Alpha Blondy,Youssou N~Dour na Koffi Olomide. die tageszeitung limeandika kwamba viongozi wa Afrika walifuatia kwa kutoa kauli zao. Mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika Alpha Conde ameitaka serikali ya Libya ichukue hatua mara moja. Niger inataka mkasa huo ujadiliwe kwenye mkutano wa viongozi wa Umoja wa Afrika na wa Umoja wa Ulaya utakaofanyika wiki ijayo nchini Cote d'voire
Na gazeti la Frankfurter Allgemeine linatilia maanani kwamba nchi za Afrika zinahitaji kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika miundo mbinu. Linasema bila ya barabara na njia nzuri za reli, bara la Afrika halitapata maendeleoya haraka. Bila ya miundombinu hayatapatikana maendeleo barani Afrika. Kiasi kikubwa sana cha fedha kinahitajika kwa ajili ya kujenga miundombinu.Lakini swali ni jee fedha hizo zitatoka wapi? Gharama kubwa za usafirishaji ni sababu mojawapo ya nchi za Afrika kushindwa kufanya biashara miongoni mwao kwa kiwango kikubwa. Pamoja na hayo linasema gazeti la Frankfurter Allgemeine, pana tatizo la nishati. Kutokana na umeme kukatika mara kwa mara wafanyabiashara wanapoteza takriban asilimia 5 ya faida zao.
Mwandishi: Zainab Aziz/Deutschen Zeitungen
Mhariri: Mohammed Khelef