Afrika katika magazeti ya Ujerumani
27 Julai 2018Frankfurter Allgemeine
Gazeti hilo linafahamisha kwamba rais Xi Jinping alifanya ziara nchini Senegal, Rwanda, Mauritius na Afrika Kusini ambako alihudhuria mkutano wa kilele wa viongozi wa nchi zinazoinukia kiuchumi. Gazeti hilo la Frankfurter Allgemeine linatilia maanani kwamba ziara ya rais wa China barani Afrika ni muhimu kwa sababu bara hilo linahitaji vitega uchumi na uhusiano wa kibiashara na nchi hiyo ambayo ni ya pili duniani kwa nguvu za kiuchumi. Frankfurter Allgemine linasisitiza kwamba wakati wote masuala ya fedha na biashara yanakuwa mbele, kiongozi wa China anapofanya ziara katika nchi za Afrika mfano ni Afrika Kusini na linaeleza:
Katika kipindi cha miaka 9 iliyopita biashara kati ya China na Afrika kusini imestawi hadi kufikia thamani ya dola bilioni 39. Gazeti hilo la Frankfurter Allgemeine linasema Afrika kusini inahitaji sana fedha kwa sababu nchi hiyo inakabiliwa na mgogoro mkubwa wa kiuchumi. Na kwa sasa wawekezaji vitega uchumi wanasita kwenda nchini humo tangu ilipotangazwa kwamba wakulima wa kizungu watanyang'anywa ardhi bila ya kulipwa fidia.
Die Zeit
Nalo gazeti la Die Zeit wiki hii linazungumzia juu ya mustakabal wa Zimbabwe linauliza iwapo watu wa nchi hiyo wanaweza kuamua juu ya mustakabal huo? Gazeti hilo linaeleza kwamba Zimbabwe ilimwondoa Mugabe mwaka uliopita. Jee watu wa nchi hiyo sasa wataweza kupiga kura kwa hiari na kuwachagua viongozi wapya. Baada ya kufanyika mapinduzi ya kiungwana, Mugabe aliondolewa na mahala pake pameshikwa na aliyekuwa makamu wake Emmerson Mnangagwa.
Gazeti hilo la Die Zeit linasema Mnangagwa mwenye umri wa miaka 75 aliisubiri fursa hiyo kwa muda mrefu na sasa anapaswa kuthibitisha kwa watu wa Zimbabwe kwamba anaweza kuwaletea mabadiliko wanayoyataka. Gazeti hilo linafahamisha kwamba hapo siku ya Jumatatu watu wa Zimbabwe watashiriki katika kupiga kura ya kuamua juu ya mustakabal wao. Dunia nzima inasubiri kwa hamu kubwa. Lakini gazeti hilo linautazama uchaguzi huo kwa macho mawili tofauti. Jicho moja linawatazama wapiga kura.Jee watamchagua kiongozi wanaemtaka kwa hiari zao? Na jicho la pili linamtazama bwana Emmerson Mnangagwa.Jee atakubali kushindwa ndapo watu wake hawatamchagua? Jibu litapatikana baada ya uchaguzi.
die tageszeitung
Gazeti la die tageszeitung ambalo limejiunga na mjadala juu ya unyanyasi wa kingono,siyo viwandani au maofsini bali kwenye taasisi zinazopaswa kutoa maadili. Gazeti hilo linatupeleka hadi Uganda ambako madai ya kunyanyaswa wanafunzi wa kike yamewashangaza wengi. Kichwa cha habari cha gazeti hilo kinasema "Malipo ya kupata cheti cha shule ni Ngono!" Gazeti hilo linaeleza kwamba kiwango cha kudhalilishwa kwa wasichana kilifichuliwa mnamo mwezi Juni katika ripoti ya kurasa 30. Kamati ya uchunguzi kwenye chuo kikuu marufu cha Makerere iliwahoji watu 234 na miongoni mwa hao asilimia 60 walikuwa wanawake. Idadi kubwa ya wanawake hao waliweza kutoa ushahidi wa kuthibitisha jinsi walivyodhalilishwa kingono na wahadhiri na maprofesa!
Ushahidi
Gazeti la die tageszeitung linafahamisha kwamba ushahidi wa kutosha ulidhihirika kwenye maziko ya profesa Lawrence Mukiibi aliyekuwa mwasisi wa mtandao wa shule na vyuo binafsi nchini Uganda. Watoto mia moja walitokea kwenye maziko ya profesa huyo. Wote ni watoto wa marehemu profesa huyo.
Familia ya marehemu imesema kuwa watoto wake waliozaliwa ndani ya ndoa ni 24 tu.Lakini wote wengine alizaa na wanafunzi wake. Rushwa imekithiri katika sekta ya elimu nchini Uganda.Ili kuruhusiwa kufanya mitihani wanafunzi wanawahonga wahusika. Akina kaka wanatoa fedha na akina dada wanalipa kwa njia nyingine. Gazeti la die tageszeitung linafahamisha katika makala yake kwamba gharama za masomo ni kubwa kwa familia nyingi nchini Uganda. Maprofesa wanaijua vizuri hali hiyo na wanaitumia kukidhi haja zao.
Stern
Gazeti la Stern wiki hii inatukumbusha methali ya kiswahili, inayosema mwenda tezi na omo marejeo ni ngamani! Methali hiyo inamhusu Anthony Mathu kutoka Kenya mwenye umri wa miaka 39. Gazeti hilo linatupasha zaidi kwamba kutokana na mambo kwenda mrama baada ya kuishi Ujerumani kwa muda wa miaka 11 mkenya huyo aliamua kurudi nyumbani. Kwanza hakumaliza masomo yake. Pili ndoa yake ilivunjika. Anthony Mathu aliamua kurudi nyumbani, miaka minne iliyopita alianza safari mpya ya maisha yake. Sasa amekuwa mfanyabiashara mwenye mafanikio na amefungua ofisi yake kwenye kitongoji cha Kitengela katika jiji la Nairobi.
Gazeti hilo la Stern linasisitiza katika makala yake kwamba karibu wakati wote habari zinazoandikwa ni juu ya vijana wa Afrika wanaojaribu kuja Ulaya ili kutafuta maisha bora lakini ustawi wa uchumi barani Afrika pia unatoa fursa nzuri za kazi.
Mwandishi. Zainab Aziz/Deutsche Zeitungen
Mhariri: Mohammed Khelef