Afrika katika magazeti ya Ujerumani
26 Oktoba 2018die tageszeitung
Mwishoni mwa wiki iliyopita ghadhabu za watu ziliripuka katika mji wa Beni, wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo baada ya watu hao kushiriki kwenye maziko. Maziko hayo yalikuwa ya raia 11 waliouliwa na watu wasiojulikana. Baada ya wahalifu kuwaua raia hao waliwateka watoto 13. Gazeti hilo la die tageszeitung linasema kama kawaida, wanajeshi wa serikali walichelewa kufika mahala pa tukio na hivyo haikuwezekana kuyazuia mauaji hayo ya halaiki.
Gazeti hilo linaeleza kuwa ghadhabu za wananchi wa mashariki mwa Kongo,zinasababishwa na ajizi inayofanywa na majeshi ya usalama, na linakumbusha kwamba mamia ya raia wameuawa katika eneo hilo la mashariki ya Kongo mnamo miaka ya hivi karibuni, na wakati mwingine baadhi ya raia hao wanauliwa mbele ya wanajeshi.
Die Welt
Gazeti la Die Welt limeandkika juu ya juhudi za kupambana na maradhi ya Ebola. Gazeti hilo limewanukulu maafisa wa shirika la afya duniani WHO wakisema hatari ya maambukizi ni kubwa katika eneo hilo la mashariki lakini siyo kwa nchi jirani. Hakuna hatari ya maradhi hayo kuenea katika nchi jirani kutokana na juhudi za kupambana nayo, ikiwa pamoja na kutoa chanjo ya aina mpya inayoleta matumaini makubwa ya kuweza kuzuia kuenea haraka kwa maambukizi ya ugonjwa wa Ebola.
Watu wote waliowahi kuwakaribia wale wenye virusi vya Ebola wanapewa chanjo. Mpaka sasa watu zaidi ya 18,000 wameshadungwa sindano hizo za kinga, miongoni mwao watoto 4000. Gazeti hilo la Die Welt linafahamisha kuwa wahusika wanahakikisha kwamba wanaougua maradhi hayo wanatenganishwa na jamii na wale wanaokufa wanazikwa haraka ili kuzuia maambukizi.
Süddeutsche
Ethiopia inaendelea na hatua ya mageuzi makubwa. Gazeti la Süddeutsche limejikita na taarifa ya kuteuliwa kwa waziri wa amani nchini humo bibi Muferiat Kamil. Gazeti linaeleza kuwa tangu kuingia madarakani kwa waziri mkuu Abiy Ahmed, mambo mengi yamebadilika nchini Ethiopia. Maalfu ya wafungwa wa kisiasa wameachiwa huru, waziri mkuu huyo amewarejesha nyumbani wapinzani waliokuwa wanaishi nchi za nje na pia ametiliana saini mkataba wa amani na Eritrea. Südeutsche linafahamisha kwamba baada ya mkataba huo wa amani kutiwa saini wizara ya amani imeundwa, itakayosimamiwa na bibi Muferiat Kamil mwenye umri wa miaka 42. Jukumu lake litakuwa kudumisha amani ndani ya nchi.
Lakini haijulikani namna mama huyo atakavyolitekeleza jukumu lake, ila gazeti hilo la Süddeutsche linatilia maanani kwamba waziri huyo wa amani anakabiliwa na kitendawili. Wakati ambapo hatua kadhaa za mageuzi zimechukuliwa na waziri mkuu Abiy Ahmed, migogoro mingi imezuka mnamo kipindi hicho. Watu wapatao milioni moja wamekimbia ghasia.
Watu wengine kadhaa waliuawa kwa kupigwa risasi na polisi na maalfu wengine walikamatwa. Gazeti la Südeutsche linasema katika makala yake kwamba baadhi ya wananchi nchini Ethiopia wanatamani kurejeshwa kwa udikteta ili utulivu udumishwe. Gazeti hilo linasema hali ni ya wasiwasi nchini Ethiopia na limewanukulu watu wanaoifananisha hali hiyo na kufunuliwa kwa mfuniko uliokuwa unazuia maji kumwagika.Jee waziri wa amani bibi Muferat Kamil ataweza kukifunika tena chungu!.
Frankfurter Allgemeine
Gazeti la Frankfurter Allgemeine linatupeleka Zambia ambako linasema, nchi hiyo inapanga mauaji lakini ni mauaji ya nini au ya nani? Linatufahamisha zaidi kwamba Zambia inapanga kuwaua viboko 2000 ili kudhibiti idadi ya wanyama hao. Na si mwengine aliyetangaza mpango huo bali ni waziri wa utalii Charles Banda. Sababu ni kwamba kina cha maji kinaendelea kushuka kwenye mto Luangwa kutokana na uhaba wa mvua na hivyo pana hatari ya wanyama hao kuhamia nchi kavu na kuleta hatari. Waziri Banda amenukuliwa akieleza kuwa hifadhi ya Luangwa kwa sasa ina viboko zaidi ya 13,000 lakini mbuga hiyo ina uwezo wa kuwahifadhi wanyama hao 5000 tu na kwa hivyo lazima wapunguzwe.
Mwandishi: Zainab Aziz/Deutsche Zeitungen
Mhariri: Mohammed Abdulrahman