1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

4 Januari 2019

Yaliyoandikwa kwenye magazeti ya Ujerumani juu ya Afrika mnamo wiki hii ni pamoja na makala ya gazeti la Die Zeit juu ya mvutano unaoendelea nchini Sudan na pia kuendelea kufungiwa huduma ya Intaneti nchini Congo.

https://p.dw.com/p/3B1kX
Sudan Khartoum - Sudans Präsident - Omar Bashir
Picha: picture-alliance/Xinhua News Agency/M. Khidir

Die Zeit

Tangu mwezi wa Novemba mwaka uliopita maalfu ya watu wamekuwa wakiandamana kupinga kupanda kwa gharama za maisha nchini humo, lakini gazeti hilo linasema maandamano hayo yanalenga shabaha ndefu zaidi gazeti bhilo linaeleza kwamba maalfu ya wananchi wa Sudan wamekuwa wanaandamana siyo tu kwa ajili ya kupinga ughali wa maisha baada ya serikali kupandisha bei ya mafuta na hivyo kusababisha ongezeko la bei za bidhaa kama mkate na dawa. 

Lakini siyo tu kuongezeka kwa bei za bidhaa hizo kumezidisha ghadhabu miongoni mwa wananchi. Watu pia wanamtaka rais Omar Al-Bashir aondoke madarakani. Ghadhabu za wananchi zilidhihirika wazi baada ya waandamanaji kuwasha moto kwenye makao makuu ya chama tawala katika moja ya miji nchini humo. Gazeti la die Zeit limeripoti kwamba polisi na wanajeshi wametumia risasi za moto na kuwaua  waandamanaji 40.Taarifa hiyo imethibitishwa na mashirika huru kadhaa. Lakini mashirika mengine yanaamini kuwa idadi ya waliouawa nchini Sudan ni kubwa zaidi.

Frankfurter Allgemeine

Gazeti la Frankfurter Allgemeine kwa mara nyingine linaturudisha katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo ambako serikali ilizifunga huduma za mitandao ya kijamii mara tu baada ya uchaguzi wa rais kufanyika tarehe 30 mwezi uliopita. Gazeti hilo limeinukulu radio Okapi ya nchini Kongo ikisema tangu Jumatatu huduma hizo zimefungwa katika miji yote mikubwa. Lakini waziri wa mawasiliano amesema hana maelezo yoyote juu ya kadhia hiyo ambayo amedai kuwa ni ya kushangaza na yaliyotokea mara tu baada ya kufanyika uchaguzi wa rais unaotarajiwa kuleta mabadiliko ya uongozi kwa njia ya kidemokrasia kwa mara ya kwanza katika historia ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Martin Fayulu kiongozi wa upinzani nchini Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo
Martin Fayulu kiongozi wa upinzani nchini Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo Picha: Getty Images/AFP/T. Charlier

Gazeti la Frankfurter Allgemeine linasema hakuna mtu yeyote anayeamini kwamba waziri huyo hakijui kilichotokea, kwa sababu hii si mara ya kwanza kwa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuzuia shughuli za internet na mitandao ya kijamii kwa jumla, kwa lengo la kukwamisha kampeni za wapinzani. Na kampuni inayotoa huduma hizo „Global pia  imesema iliambiwa na serikali izifunge huduma zake. 

Kiongozi wa upinzani Martin Fayulu anatuhumu kwamba serikali imeifunga mitandao ya kijami ili iweze kupata ushindi mkubwa kwa njia ya wizi.  Wakati huo huo kiongozi mwingine wa upinzani Felix Tshisekedi na mgombea wa chama tawala cha umma, bwana Emmanuel Ramazan Shadary, kila mmoja anadai kushinda. Gazeti hilo la Frankfurter Allgemeine limesema ni vigumu kuamini iwapo tume ya uchaguzi itatangaza matokeo kamili tarehe 15 hasa kutokana na kubainika kwamba mashine za kupigia kura ziliharibika zaidi ya mara mia tano. 

Neue Zürcher

Nchini Burundi. Gazeti la Neue Zürcher linatufahamisha kwamba serikali ya nchi hiyo imeamua kuhamia katika mji mkuu mpya unaoitwa Gitega. Mji huo mdogo una wakaazi 40,000, soko moja, kanisa na nyumba ya makumbusho inayohitaji kufanyiwa ukarabati.  Hadi sasa mji huo mdogo ulikuwa kituo cha mapunziko kwa ajili ya wasafiri lakini hadhi ya mji huo huenda ikabadilika baada ya rais Pierre Nkurunziza kutangaza, muda mfupi tu kabla ya Krismasi kwamba mji mdogo wa Gitega kuanzia sasa ndiyo utakaokuwa makao makuu ya serikali.

Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza
Rais wa Burundi Pierre NkurunzizaPicha: Reuters/E. Ngendakumana

Viongozi wa serikali watakuwa wanafanya vikao katika mji huo na wizara tano zitahamia katika miezi michache ijayo. Gazeti la Neue Zürcher linasema sababu ya rais Nkurunziza kufanya uamuzi huo ni kwamba mji wa Gitega upo kati kati ya Burundi. Mji mkuu wa sasa Bujumbura ambao kwa sasa una wakaazi wapatao milioni 1 na laki mbili uko magharibi mwa Burundi.

Gazeti hilo linasema uamuzi huo  umesababisha sintofahamu na linaeleza kwamba zipo sababu nyingi za kuupinga uamuzi huo. Kwanza mji huo mdogo wa Gitega unahitaji  kujengewa miundombinu kwa ajili ya makao makuu ya serikali na wizara. Baadhi ya watu wanaamini kwamba rais Nkurunziza ameamua kuuhamisha mji mkuu kwa sababu ya kuwahofia wapinzani wenye nguvu kubwa katika mji wa Bujumbura. Gazeti la Neue Zürcher limewakariri  wapinzani wakisema kuwa Nkurunziza amefanya uamuzi wa kuuhamishia mji mkuu katika mji wa Gitega ili kuleta kumbukumbu ya enzi ya ufalme.

Mwandishi:Zainab Aziz/Deutsche Zeitungen

Mhariri: Sekione Kitojo