1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Al-Sisi aanza muhula wa tatu baada ya uokozi wa kiuchumi

1 Aprili 2024

Rais wa Misri Abdel Fattah anaanza muhula wake wa tatu wiki hii akitiwa matumaini na ufadhili mpya mkubwa, lakini wataalamu wanaonya kuwa safari ya kutoka kwenye mzozo wa kiuchumi bado ni ndefu.

https://p.dw.com/p/4eJRV
Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi
Rais Abdel Fattah al-Sisi aanza muhula wake wa tatu wa miaka sita wiki hii.Picha: John Macdougall/AP Photo/picture alliance

Sisi alishinda uchaguzi wa rais wa Desemba kwa asilimia 89.6 ya kura, akishindana dhidi ya watu watatu wasiojulikana. Anatazamiwa kuanza muhula wake wa tatu rasmi siku ya Jumatano, huku vyombo vya habari vya nchini humo vikiripoti kwamba ataapa mbele ya bunge siku moja kabla.

Muhula huu wa miaka sita unatazamiwa kuwa wa mwisho kwa Rais Al-Sisi mwenye umri wa miaka 69, endapo hakutofanyika marekebisho mengine ya katiba kuongeza muda wake wa kukaa madarakani.

Wataalamu wa mambo wamezungumzia uwezekano wa mabadiliko ya baraza la mawaziri wakati Cairo inajitahidi kudhibiti athari za mzozo mbaya wa kiuchumi uliodumu kwa miaka miwili na uhaba mkubwa wa fedha za kigeni.

Mwanzoni mwa mwaka 2024, taifa hilo lenye wakazi wengi zaidi katika ulimwengu wa Kiarabu lilionekana kuelemewa na kuelekea kushindwa kulipa madeni yake na kuporomoka kwa uchumi, wachambuzi walisema, kabla ya kupokea kwa ghafla zaidi ya dola bilioni 50 za mikopo na uwekezaji.

Rais wa Misri Al-Sisi na Amir wa UAE Sheikh Muhammmad bin Zayid
Rais Abdel Fattah Al-Sisi, kulia, akisalimiama na Rais wa Umoja wa Falme za Kiarabu, UAE, Sheikh Mohammad bin Zayid al-Nahyan. UAE imeisaida Misri kwa ufadhili mkubwa wa kifedha na kuimarisha uchumi wake.Picha: OFFICE OF THE EGYPTIAN PRESIDENT/dpa/picture alliance

Ndani ya wiki kadhaa, Umoja wa Falme za Kiarabu ulitangaza mpango wa dola bilioni 35 wa maendeleo ya ardhi kwa ajili ya Rasi ya Misri ya al-Hikma, huku Shirika la Fedha la Kimataifa, IMF, likiongeza zaidi ya mara mbili, mkopo wa dola bilioni 3, na Benki ya Dunia na Umoja wa Ulaya wakisaini mikataba mipya ya ufadhili.

Uokoaji huo mkubwa umeinusuru Misri  dhidi ya "kutumbukia kwenye shimo", kulingana na naibu waziri mkuu wa zamani Ziad Bahaa-Eldin. Kufuatia makubaliano hayo na kupunguzwa tena kwa thamani ya sarafu ya Misri - kwa mara ya tano tangu 2016 -- viashiria vya kiuchumi vilionekana kuboreka.

Makampuni ya huduma za kifedha yalipandisha viwango vya ukopeshekaji wa Misri, huku orodha ya miezi kadhaa iliyozuiliwa ikianza kutolewa katika uchumi wa taifa hilo unaotegemea uagizaji wa nje.

Wachambuzi wanaamini mgogoro bado haujaisha

Lakini "hatupaswi kuamini kwamba mgogoro umepita, au kwamba matatizo yetu yametatuliwa," aliandika Bahaa-Eldin katika toleo la hivi karibuni la gazeti binafsi la Al-Masry Al-Youm.

Soma pia: Misri yapandisha bei ya mafuta kufuatia kushuka kwa thamani ya sarafu

Mizizi ya mgogoro wa Misri -- ikiwa ni pamoja na "kasi ya matumizi ya fedha za umma, uwezo wa serikali kwenye uchumi, na kiwango cha mfumuko wa bei" -- lazima ishughulikiwe, mchambuzi wa uchumi na mbunge wa zamani Mohamed Fouad aliiambia AFP.

Wiki hii, Wamisri watamtazama Sisi akila kiapo kutokea Mji Mkuu Mpya wa Utawala -- ambao ni mradi wenye utata uliogharimu dola bilioni 58 katika jangwa mashariki mwa Cairo -- huku watu wengi wakihangaika kujikimu katikati mwa mfumuko wa bei wa asilimia 35.

Misri Cairo 2023 | Uchaguzi wa Rais | Rais Abdel Fattah al-Sisi akipiga kura yake
Rais Al-Sisi ataapishwa kutokea mji mkuu mpya wa kiutawala uliogharimu mabilioni ya dola licha ya Wamisri kukabiliwa na hali ngumu ya maisha.Picha: Egyptian Presidency Media Office via AP/picture alliance

Uokoaji huo mkubwa zaidi kuliko ilivyotarajiwa, umekuja na masharti kwa Cairo, ambayo ni kuhamia kwenye viwango mwafaka vya ubadilishaji fedha na "kuiondoa serikali na jeshi kwenye shughuli za kiuchumi", kulingana na mkuu wa IMF Kristalina Georgiaieva.

Lakini wachambuzi wameonya kuwa huenda serikali bado inaibeba pauni ya Misri. Na kulingana na Fouad, "serikali inataka kuingilia kati zaidi, sio kujiondoa" kutoka kwenye shughuli za kiuchumi.

Wasiwasi umeongezeka kwamba, bila mageuzi makubwa -- ambayo serikali imeapa kuyafanya -- Misri inaweza kujikuta katika mzunguko mpya wa mgogoro. "Ili kuepuka kurudia makosa, tunahitaji mabadiliko ya ubora katika namna tunavyosimamia uchumi wetu halisi," kulingana na Bahaa-Eldin.

Soma pia: Umoja wa Ulaya kuimarisha uhusiano na Misri kwa kutoa ufadhili wa mabilioni dola

Wakati huo huo, Misri inajikuta ikikabiliwa na athari za kikanda kutokana na vita viwili kwenye mipaka yake. Kutoka jirani yake wa Sudan, zaidi ya wakimbizi nusu milioni wameingia Misri, wakikimbia vita kati ya jeshi la serikali na wanamgambo wa kundi la RSF.

Na katika Ukanda wa Gaza, Wapalestina milioni 1.5 wametafuta hifadhi katika mji wa Rafah, uliobanwa kati ya mpaka wa Misri kwa upande mmoja na mashambulizi ya mara kwa mara ya Israel kwa upande mwingine.

Misri | Mkuu wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya von der Leyen na Rais Al-Sisi
Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen akiwa na Rais Al-Sisi mjini Cairo. Umoja wa Ulaya pia umesaini makubaliano ya ufadhili na Misri.Picha: The Egyptian Presidency/REUTERS

Wamisri zaidi wapambana kumudu maisha

Ndani ya taifa hilo la wakaazi milioni 106 theluthi mbili ya watu wanapambana kumudu maisha yao, wakiwa wameishi kwenye, au chini ya mstari wa umaskini hata kabla ya mgogoro wa sasa.

"Watu walikuwa tayari wamechanganyikiwa kwa sababu walidhani hakuna suluhu," kulingana na Mohamed Lotfy, mkurugenzi mtendaji wa Tume ya Haki na Uhuru ya Misri (ECRF). Lakini mtiririko mkubwa wa ufadhili unaweza kuwarejeshea matumaini, watatarajia mambo kuboreka," aliiambia AFP.

"Ikiwa haitakuwa hivyo, watu watahisi kama wamejitolea na kusubiri na kufuata sheria, lakini hawana chochote cha kuonyesha kwa kujitolea kwao - kwa kuwa bado watakuwa hawana uwezo wa kuishi."

Licha ya baadhi ya Wamisri kutangaza hisia zao za kufadhaika na kukatishwa tamaa kwenye mitandao ya kijamii, nafasi ya upinzani wa umma imeminywa pakubwa.

Katika muongo mmoja uliopita, Cairo imeendesha kile ambacho Lotfy anakiita "vita vya msukosuko" dhidi ya mashirika ya kiraia -- kwa kuwatia kizuizini makumi ya maelfu ya watu, kushtaki makundi ya kutetea haki za binadamu na kutokomeza karibu upinzani wote.

Meli kubwa yakwama katika mfereji wa Suez

Ingawa matumaini ya mafanikio yalionekana mwaka 2022, baada ya Sisi kuzindua mpango wa "majadiliano ya kitaifa" na kuanza kuwaachilia wafungwa wa kisiasa wenye hadhi ya juu -- "matumaini hayo yote yalikatizwa hivi karibuni," Lotfy alisema.

Sasa, wakati ambapo idadi ya watu waliozuwiliwa ikipindukia maradufu, kwa mujibu wa idadi ya ECRF, Lotfy anasema rekodi ya haki za binadamu ya Misri, "inasalia kuwa janga" wakati ambapo hisia za kukata tamaa zikiendelea kuikumba nchi hiyo.

Chanzo: AFPE