1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ANKARA: Bunge lapitisha tarehe ya uchaguzi

3 Mei 2007
https://p.dw.com/p/CC57

Bunge la Uturuki limepitisha bila ya kupingwa tarehe 22 mwezi Julai kuwa ndio siku ya uchaguzi mkuu kama ilivyo pendekezwa na tume ya katiba ya bunge la nchi hiyo.

Uchaguzi huo utafanyika mwezi mmoja baada ya muda uliopendekezwa hapo awali na waziri mkuu Recep Tayyip Erdogan na chama chake cha kihafidhina cha AKP.

Muelekeo huu unadhaniwa kuwa ndio utatatua mzozo wa kisiasa unaoikumba Uturuki baada ya mahakama ya katiba kubatilisha kura ya bunge ya kumchagua rais mpya.

Mahakama hiyo ilibatilisha matokeo ya duru ya kwanza ya uchaguzi uliofanyika ijumaa iliyopita baada ya matokeo hayo kukataliwa na upande wa upinzani.

Mgombea wa urais wa pekee alikuwa waziri wa mambo ya nje bwana Abdullah Gul.