Guterres: Aomba Somalia na Ethiopia wasuluhishe tofauti zao
21 Januari 2024Akizungumza mjini Kampala anakohudhuria mkutano wa kilele wa G77 pamoja na China, Guterres amesema kupitia mazungumzo ndiko kutakapopatika suluhu ya mzozo uliopo.
Wasiwasi umeonekana katika pembe hiyo ya Afrika tangu nchi isiokuwa na bahari ya Ethiopia kuwa na makubaliano na Somaliland mnamo Januari mosi yanayoipa Ethiopia nafasi ya kutumia bahari ya shamu na badala yake nchi hiyo ilitambue jimbo hilo kama taifa huru.
Siku ya Alhamisi Somalia iliondoa uwezekano wa aina yoyote wa kuwa na mazungumzo na Ethiopia hadi pale makubaliano hayo yatakapofutwa na kuapa kupambana kuupinga.
Somalia yasema hakuna nafasi ya upatanishi kati yake na Ethiopia
Kwengineko rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi amesema nchi yake haitokubali kitisho chochote dhidi ya Somalia au usalama wake, baada ya Ethiopia kusema itazingatia kutambua madai ya uhuru wa Somaliland.
Katika mkutano na waandishi habari mjini Cairo akiwa pamoja na rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud, al Sisi amesema hatua ya taifa fulani kutaka kurukia ardhi ya watu na kutaka kuidhibiti ni kitu ambacho hakuna atakayekubaliana nacho.
Somaliland ilijitangaza kuwa huru kutoka Somalia mwaka 1991 lakini bado haijatambuliwa na hata nchi moja duniani kuwa nchi huru.