Askari wawili wa Afrika Kusini wauawa katika mlipuko Kongo
15 Februari 2024Jeshi la Ulinzi wa taifa la Afrika Kusini, ambalo linasimamia vikosi vyote vya jeshi la nchi hiyo, limesema linaamini kuwa mlipuko wa kombora hilo siku ya Jumatano ulitokana na "ufyetuaji usio wa moja kwa moja" na kwamba uchunguzi unaendelea kubaini ni nani aliyehusika.
Afrika Kusini imepeleka wanajeshi nchini Kongo kama sehemu ya ujumbe wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika, SADC, kupambana dhidi ya makundi ya waasi mashariki mwa nchi hiyo.
Afrika Kusini ilitangaza wiki iliyopita kwamba itatuma kikosi kipya cha wanajeshi 2,900 mashariki mwa Kongo. Haikubainika wazi mara moja ikiwa waliouawa na kujeruhiwa walikuwa sehemu ya kikosi hicho kipya.
Kambi iliyopigwa na kombora hilo iko katika mkoa wa Kivu Kaskazini, alisema Siphiwe Dlamini, msemaji wa jeshi la ulinzi wa taifa la Afrika Kusini. Askari waliojeruhiwa walipelekwa hospitalini katika mji wa Goma.
Soma pia: DRC: Maelfu wakimbia makwao kufuatia mapigano makali Goma
Vurugu katika eneo hilo lenye utajiri wa madini zimeongezeka katika wiki za karibuni, huku wengi wakilaumu mashambulizi kwa kundi la waasi la M23, ambalo limekuwa likipigana dhidi ya wanajeshi wa Kongo katika eneo hilo kwa miaka kadhaa.
Hofu ya kuutwa mji wa Goma
Serikali ya Kongo inasema M23 inapokea msaada wa kijeshi kutoka nchi jirani ya Rwanda, jambo ambalo Rwanda inakanusha.
Lakini M23 imedokeza katika taarifa za hivi kakribuni kwamba iko katikati ya hatau mpya za kusonga mbele mashariki mwa Kongo, na kusababisha hofu kuwa kundi hilo linaulenga tena mji wa Goma, ambao liliwahi kuuteka miaka 10 iliyopita.
Zaidi ya watu milioni 1 wamekimbia makazi yao kutokana na mzozo huo tangu Novemba, mashirika ya misaada yanasema. Hiyo inaongezea kwa milioni 6.9 ambao tayari wamekimbia makazi yao katika moja ya majanga makubwa zaidi ya kibinadamu ulimwenguni.
Siku ya Alhamisi, Baraza la Wakimbizi la Norway lilisema kusonga mbele kwa makundi yenye silaha kuelekea mji muhimu wa Sake, karibu na Goma, "kunaleta tishio kwa mfumo mzima wa misaada" mashariki mwa Kongo.
Soma pia: Hofu yaongezeka Kongo baada ya M23 kudhibiti mji unaonganisha Goma na Bukavu
"Kutengwa kwa Goma, makazi ya zaidi ya watu milioni 2 na kuwakaribisha mamia kwa maelfu ya watu waliokimbia makazi yao ambao wamekimbia mapigano na makundi yenye silaha, kunaweza kuleta matokeo mabaya katika eneo hilo," NRC ilisema.