Ayatullah Ali Khamenei atetea kuishambulia Israel
4 Oktoba 2024Kwenye hotuba hiyo mbele ya mamia kwa maelfu ya watu waliokusanyika kwenye msikiti mkuu wa Imam Khomeini Mosalla mjini Terhan, Khamenei amesema shambulizi lililoilenga Israel lilikuwa halali kisheria na kwamba upinzani dhidi ya dola hiyo hautakoma.
Kiongozi huyo mkuu Iran pia ameyasifu makundi ya Hezbollah na Hamas yanayopigana na Israel nchini Lebabon na Ukanda wa Gaza, akisema yanafanya hivyo kulinda maslahi ya kanda nzima.
Soma zaidi: Iran yawaita mabalozi wa Ulaya baada ya kuikosoa kufuatia shambulizi lake dhidi ya Israel
Makundi hayo mawili yameorodheshwa kuwa ya kigaidi kwenye mataifa mengi ya Magharibi na Israel inaendesha kampeni ya kijeshi inayodai ina nia ya kuyasambaratisha.
Hotuba ya Khamenei wakati wa ibada ya Ijumaa ambayo ni ya kwanza katika kipindi cha miaka mitano, imetolewa wakati wasiwasi unaongezeka kwamba kanda ya Mashariki ya Kati ipo ukingoni wa kutumbikia kwenye vita kamili.