Azerbaijan: Urusi kuwaadhibu waliohusika na ajali ya ndege
30 Desemba 2024Matangazo
Ndege hiyo ya shirika la ndege la Azerbaijan ilianguka Kazakhstan mnamo Disemba 25, na kuua watu 38 kati ya 67 waliokuwa ndani. Rais wa Azerbaijan Ilham Aliyev ameitaka Moscow ikubali kuwajibika kwa kuidungua ndege hiyo kimakosa ilipojaribu kutua katika uwanja wa ndege wa Grozny kusini mwa Urusi. Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Azerbaijan amesema katika taarifa yake leo kwamba mkuu wa Kamati ya Uchunguzi ya Urusi amewaambia kwamba Urusi inachukua hatua kali kuwabaini watu walio na hatia na kuwafikisha kwenye mikono ya sheria. Siku ya Jumamosi, Rais wa Urusi Vladmir Putin aliomba msamaha kwa Aliyev baada ya ajali hiyo ililiyotokea karibu na mji wa pwani wa Aktau nchini Kazakhstan.