Baada ya miaka sita mkutano wa mazingira warejea Afrika
3 Novemba 2022Mkutano huo unajiri baada ya miaka sita na mikutano minne iliyofanyika barani Ulaya.
Mkutano huo huo wa 27 unaofanyika kila mwaka na kuwaleta pamoja wadau wa mazingira kutafuta juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi unaojulikana kama COP27 utafanyika katika mji wa mapumziko wa Sharm el-Sheikh nchini Misri kuanzia wiki ijayo.
Mkutano huu umepewa jina la "COP ya Afrika" huku maafisa na wanaharakati wakitumai kwa Afrika kuwa mwenyeji wa mkutano huo mkubwa wa mazingira kunamaanisha masilahi ya bara hilo yatawasilishwa vyema katika majadiliano kuhusu tabia nchi yatakayofanyika.
Katika mkutano wa COP26 mwaka uliopita, karibu nchi 200 duniani zilikubali kuwasilisha ahadi, mipango na mikakati ya kupunguza utoaji wa gesi ya ukaa kwa ngazi ya taifa kabla ya mkutano wa wiki ijayo wa COP27.