BANDAH ACEH: Rais Yudhoyono aamuru wanajeshi kukomesha mashambulio yao dhidi ya waasi
21 Julai 2005Matangazo
Rais wa Indonesia, Susilo Bambang Yudhoyono ameviamuru vikosi vya wanajeshi katika mkoa wa Aceh kukomesha mashambulio yao dhidi ya waasi ili kuuheshimu mkataba mpya wa amani. Amelitoa tangazo hilo baada ya waasi kuwalaumu wanajeshi wa serikali kwa kuongeza mashambulio dhidi yao, hata licha ya mkataba huo kufikiwa mnamo Jumapili iliyopita.
Watu 11 wameuwawa mkoani humo tangu serikali na waasi walipofikia maakubaliano ya amani mjini Helsinki, nchini Finland, siku nne zilizopita. Mkataba huo, ambao utasainiwa rasmi mwezi Agosti, unalenga kumaliza miongo mitatu ya machafuko katika mkoa wa Aceh, ambayo yamesababisha vifo vya watu elfu 15.