Baraza Kuu UM lataka usitishaji mapigano mara moja Gaza
13 Desemba 2023Mataifa ya Kiarabu na yenye idadi kubwa ya Waislamu yalikuwa yameitisha kikao cha dharura cha Baraza hilo lenye nchi 193 wanachama kwa ajili ya kura hiyo iliyopigwa usiku wa kuamkia Jumatano (13 Disemba).
Akizungumza muda mfupi kabla ya kura hiyo kupigwa, Balozi wa Palestina katika Umoja wa Mataifa, Riyad Mansour, alisema kuwa mataifa hayo yalikuwa yamefanya kampeni kuhamasisha uungwaji mkono wa azimio lililopitishwa.
Nchi 153 zimeliunga mkono azimio hilo, huku 10 tu zikilipinga. Kumi hizo zilizopiga kura ya hapana ni Marekani na Israel, zikiungwa mkono na Jamhuri ya Czech - ambayo imebadilisha jina na kuitwa Czechia - Austria, Guatemala, Liberia, Micronesia, Nauru, Papua New Guinea, na Paraguay.
Soma zaidi: Baraza kuu la Umoja wa Mataifa latarajiwa kutoa wito wa kusitishwa kwa mapigano katika ukanda wa Gaza
Ujerumani ni miongoni mwa nchi 23 ambazo zimejizuia kupiga kura.
Katika ujumbe uliochapishwa katika mtandao wa X ambao zamani ulijulikana kama Twitter, wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani imesema nchi hiyo haikuwa na chaguo jingine.
Ilisema ingawa Ujerumani inataka kumalizika kwa mateso yasiyovumilika kwa watu wa Israel na Palestina, azimio la jana lilitaka usitishaji mapigano wa jumla jamala, bila kutaja haki ya Israel kujilinda, na shambulizi la kigaidi la Hamas dhidi ya Israel la tarehe 7 Oktoba.
Umuhimu wa azimio
Ingawa azimio lililopitishwa katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa halina uzito wa kisheria kama lile la Baraza la Usalama, linabeba ujumbe muhimu wa maoni ya wengi duniani.
Azimio hilo limeonyesha kutengwa kwa Marekani na msimamo wake wa kukaidi miito ya kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza.
Marekani huchukuliwa kama upande pekee unaoweza kuishawishi Israel kusitisha mashambulizi, kwa sababu ndio mshirika wake mkuu na pia msambazaji wake wa zana za kivita.
Soma zaidi: Israel yakanusha kutaka kuwahamishia Misri wakaazi wa Gaza
Ukweli mwingine uliodhihirishwa na azimio hilo ni mgawanyiko baina ya nchi za Magharibi na sehemu nyingine za dunia ambazo zinajulikana kwa pamoja kama Upande wa Kusini mwa Dunia.
Lakini pia limeonyesha mpasuko wa kimaoni katika nchi za Ulaya. Wakati Uingereza imeungana na Ujerumani katika kujizuia, nchi kama Ufaransa na Ugiriki zimeunga mkono azimio hilo linalotaka usitishwaji mapigano kwa sababu za kibinaadamu katika Ukanda wa Gaza.
Hapo jana Rais Joe Biden wa Marekani alisema waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anapaswa kuibadilisha serikali yake yenye msimamo mkali, na kumuelezea kiongozi huyo wa Israel kama mtu asiyetaka suluhisho la mataifa mawili linaloungwa mkono na Marekani na nchi nyingine nyingi.
Aidha, katika kile kinachotazamwa kama ukosoaji mkali zaidi wa Biden dhidi ya Israel tangu kuanza kwa mzozo wa sasa, rais huyo wa Marekani amesema Israel inazidi kupoteza uungwaji mkono kimataifa kutokana na mashambulizi yake dhidi ya Hamas katika Ukanda wa Gaza, ambayo yameuwa maelfu ya raia wa Kipalestina.
Vyanzo: dpa, AP