Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kujadili mzozo wa Gaza
8 Desemba 2023Wakati jeshi la Israel likiendelea na mashambulizi yake katika Ukanda wa Gaza hasa katika miji ya Jabalia na Khan Younis, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linakutana Ijumaa baada ya Katibu Mkuu Antonio Guterres kutumia Kifungu cha 99 cha Mkataba wa Umoja wa Mataifa, ambacho kwa miongo kadhaa hakijatumiwa. Kifungu hicho kinamruhusu katibu mkuu kuwasilisha kwa baraza la Usalama suala lolote ambalo kwa mtazamo wake linaweza kutishia amani na usalama kimataifa.
Soma pia:Marekani yasema Hamas walitumia hospitali kutekeleza operesheni
Guterres anatarajia kupitishwa kwa azimio la usitishwaji mapigano kwa sababu za kibinadamu ili kuzuia janga lenye athari zisizoweza kudhibitiwa kwa Wapalestina na hata kwa eneo zima la Mashariki ya Kati. Lakini Marekani tayari imeeleza kuwa haitaunga mkono hatua kama hiyo.
Nayo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani imesema "amani ya kudumu haitawezekana" ikiwa Hamas itaendeleza mashambulizi yake kutokea Ukanda wa Gaza. Msemaji wa wizara hiyo amesema Hamas inawajibika kwa vifo vya raia kwa sababu inawatumia kama ngao na kwamba kundi hilo ni tishio kwa raia wa Palestina na Israel.
Hali mbaya ya kibinaadamu Gaza
Mratibu wa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) Stephen Ryan amesema wakaazi wa Gaza wanaendelea kuteseka kwa kiwango "kisichokubalika" na kwamba mapigano huko Gaza yanazuia mashirika ya misaada kuendelea kuwasaidia watu wenye uhitaji.
Soma pia:WHO yaitaja hospitali ya Al Shifa kama "eneo la kifo"
Hali kama hiyo imeelezwa pia na Shirika la Afya Dunia WHO ambalo limeonya kuhusu kusambaratika kwa mfumo wa afya huko Gaza. Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi, Msemaji wa WHO Christian Lindmeier amesema:
"Kiuhalisia ni kwamba hali huko Gaza haielezeki. Mfumo wa afya umesambaratika. Gaza haiwezi kumudu kupoteza kituo chochote cha afya, gari ya wagonjwa au hospitali nyingine. Yanashuhudiwa matukio ya kutisha ambayo watu wakiwemo watoto wanaoomba na kulilia maji. Tumefikia katika kiwango ambacho vifaa vya kawaida na vya kimsingi havipatikani tena."
Shirika la Umoja wa Mataifa la misaada ya kibinadamu OCHA limesema ni hospitali 14 tu kati ya 36 za Ukanda wa Gaza ndizo zinazofanya kazi kikamilifu.
Soma pia: Uvamizi wa Israel katika hospitali ya Gaza wazusha wasiwasi wa kimataifa
Vita vilizuka Gaza baada ya wanamgambo wa Hamas kushambulia kusini mwa Israel Oktoba 7, na kuua takriban watu 1,200 na kuwachukua mateka watu wengine zaidi ya 200. Mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Israel yamesababisha vifo vya watu 17,177, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, kwa mujibu wa wizara ya afya inayodhibitiwa na Hamas.
Idadi hiyo ya vifo haikuweza kuthibitishwa na vyanzo huru, lakini Umoja wa Mataifa na mashirika ya haki za binadamu yanasema takwimu hizo zinaonekana kuwa sahihi. Mapigano ya wiki kadhaa yamepelekea sehemu kubwa ya Gaza kuwa magofu.