Baraza la Katiba laidhinisha kujiuzulu Bouteflika
3 Aprili 2019Kituo cha televisheni ya taifa kimeripoti kwamba baraza hilo lililijulisha bunge juu ya hatua hiyo na kutangaza nafasi ilioachwa wazi na rais wa Jamhuri ya taifa hilo la Afrika Kaskazini.
"Leo kikao chetu kinahusu kutangaza nafasi ilioachwa wazi kufuatia kujiuzulu rais wa Jamhuri bwana Abdelaziz Bouteflika hapo jana," alisema rais wa Baraza la Katiba Tayeb Belaiz alipoufungua mkutano wa leo wa wanachama 12 wa baraza lake.
Raia wa Algeria waliamkia kipindi kipya kisichokuwa na uhakika baada ya kuondoka Bouteflika aliyewaongoza kwa miaka 20, na mtu muhimu katika ulimwengu wa kisiasa katika mataifa ya kiarabu.
Kwa sasa mshirika wa Bouteflika aliye na miaka 77 ambaye ni spika wa bunge Abdelkader Bensalah ndiye aliyechukua usukani kama kiongozi wa mpito wa taifa hilo, lakini hilo linasemekana huenda likawakasirisha waandamanaji waliomuondoa Bouteflika madarakani na wanaotaka kuuondoa kabisa utawala wanaouaona kuwa wa siri na uliojaa ufisadi.
Waandamanaji wataka mfumo mzima wa serikali ya Bouteflika kuondolewa
Waandamanaji nchini humo wana wasiwasi kwamba wale watakaokuwa na jukumu la kukiendesha kipindi cha mpito ni watu waliokaribu sana na mfumo usioaminiwa wa uongozi akiwemo Waziri Mkuu Noureddine Bedoui, anayeshutumiwa kufanya udanganyifu katika uchaguzi mkuu uliopita mwaka 2014 na kuhusika katika kamata kamata ya waandamanaji wa maandamano yaliopita.
Maandamano mapya yamepangwa kufanyika siku ya Ijumaa baada ya maandamano sita ya kila ijumaa na mkusanyiko wa pamoja wa amani ulioushangaza uongozi uliokuwepo kufuatia nguvu yao na uvumilivu.
Hata hivyo vuguvugu la maandamano kwa sasa halina sauti moja juu ya mfumo wa sasa wa kisiasa.
Suali jengine linaloulizwa ambalo ni muhimu, ni juu ya ushawishi wa jeshi na je kundi la Bouteflika litachukua hatua gani inayofuata. Mkuu wa jeshi Ahmed Gaid Salah alionekana kuchochea kuondoka kwa Bouteflika kwa kutangaza kuwa hayuko imara kiafya kuendelea na majukumu ya uongozi.
Kwa wakati huu mataifa mengi duniani yanafuatilia kwa karibu hali ya kisiasa nchini Algeria na kuangalia iwapo hatua ya kukabidhiana madaraka inaweza kuwa na athari yoyote katika usafirishaji gesi na mafuta barani ulaya, Cuba na katika baadhi ya Mataifa ya Afrika au labda kuathiri ushirikiano wa kiusalama baina ya taifa hilo na Ulaya au Marekani. Msemaji wa bunge la Urusi Dmitry Peskov ameonya dhidi ya mataifa ya kigeni kuingilia siasa za ndani za Algeria.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema anatazamia kuwepo kwa mfumo wa amani na wa kidemokrasia wa kubadilishana madaraka baada ya kujiuzulu kwa Bouteflika.
Mwandishi: Amina Abubakar/AP/Reuters
Mhariri: Yusuf Saumu