Baraza la Usalama la UN kukutana kuhusu mzozo wa Haiti
6 Machi 2024Makundi ya magenge yenye silaha yanayodhibiti maeneo makubwa ya nchi yalitangaza juhudi za pamoja kumuondoa madarakani Henry na kuanza kushambulia uwanja wa ndege, magereza, vituo vya polisi na maeneo mengine ya kimkakati tangu wakati huo.
Kiongozi wa genge mwenye nguvu Jimmy Cherizer, ambaye ni afisa wa zamani wa polisi aliewekewa vikwazo na Umoja wa Mataifa kwa tuhuma za ukiukaji wa haki za binadamu, alisema ikiwa waziri mkuu Henry hatajiuzulu na iwapo jumuiya ya kimataifa itanedelea kumuunga mkono watakuwa wanaelekea kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewevitakavyosababisha mauaji ya kimbari.
"Ama Haiti inakuwa pepo au jahanamu kwetu sote. Haiwezekani kikundi kidogo cha matajiri wanaoishi katika hoteli kubwakuamua hatima ya watu wanaoishi katika vitongoji vya wafanyakazi," alisema Cherizer.
Wakati mzozo wa hivi karibuni katika taifa lililokumbwa na ghasia la Karibian ukizidi, milio ya risasi ilizuwia baadhi ya safari za ndege katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Toussaint Louverture katika mji mkuu wa Haiti. Henry alikataliwa kuingia katika nchi jirani ya Jamhuri ya Dominika, kulingana na shirika la habari la Dominic la CDN.
Soma pia: Watu kadhaa wauawa Haiti baada ya Gereza Kuu kuvamiwa
Msemaji wa ofisi ya gavana wa Puerto Rico Sheila Anglero, alisema Jumanne jioni kwamba ndege ya Henry ilikuwa imetua jimboni humo kwa muda lakini akalimbia shirika la habari la AFP kwamba hakuwa na uhakika iwapo alikuwa bado yupo.
Muafaka wa kugawana madaraka na upinzani
Henry ambaye amekuwa madarakani tangu kuuawa kwa rais Jovenel Moise mwaka wa 2021, alipaswa kuachia ngazi mwezi Februari lakini badala yake aliafiki makubaliano ya kugawana madaraka na upinzani hadi uchaguzi mpya utakapofanyika.
Maafisa wa Haiti wamekuwa wakiomba kwa miezi kadhaa msaada wa kimataifa kusaidia vikosi vyao vya usalama vilivyoelemewa, wakati magenge yakisogea kutoka mji mkuu kuelekea maeneo ya vijijini. Serikali imetangaza hali ya hatari na amri ya kutotoka nje usiku, ambayo imeongezwa hadi Jumatano.
Henry alikuwa amesafiri hadi nchini Kenya kushinikiza kutumwa kwa ujumbe wa polisi wa kimataifa unaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa kusaidia kuleta utulivu nchini mwake wakati jaribio la kumwondoa madarakani lilipoanza.
Soma pia: Haiti kujadili na Kenya juu ya kupelekwa askari
Wakati akiwa nje ya nchi, magenge ya wahalifu yalivamia magereza mawili mawili mjini Port-au-Prince, katika mashambulizi yaliosababisha vifo vya watu kadhaa na kutoroka kwa maelfu ya wafungwa.
Akitiwa wasiwasi na hali ya usalama inayozidi kudorora, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, alitoa wito wa kuchukuliwa kwa hatua za haraka wiki hii, hasa kutoa msaada wa kifedha kwa ajili ya ujumbe wa kimataifa wa kusaidia usalama.
Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa nchini Haiti Maria Isabel atahutubia mkutano wa Baraza la Usalama kwa njia ya mtandao wakati wa kikao chake cha ndani leo mchana.