Benki ya Dunia kutathmini uharibifu wa bwawa la Kakhovka
8 Juni 2023Mkurugenzi mkuu wa mipango katika ya Benki ya Dunia Anna Bjerde, amesema uharibifu wa bwawa la Novo Kakhovka umekuwa na matokeo mabaya kwa utoaji wa huduma muhimu pamoja na mazingira.
Bjerde amesema tathmini hiyo mpya itajikita kwenye uharibifu wa miundombinu na majengo ya Ukraine, huku akikadiria kuwa itagharimu dola bilioni 411 ili kuufufua upya uchumi wa Ukraine baada ya uvamizi wa Urusi.
Waziri Mkuu wa Ukraine Denys Shmyhal, ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa Twitter kuwa amefanya mazungumzo na Bjerde kuhusu athari za kuharibiwa kwa bwawa hilo, na kwamba afisa huyo alimhakikishia kuwa Benki ya Dunia itafanya tathmini ya haraka ya uharibifu na mahitaji.
Soma pia: Erdogan ashauri kuunda tume kuchunguza mkasa wa bwawa
Raia wa Ukraine wanaendelea kuyahama makazi yao kutokana na mafuriko yanayolikumba eneo la kusini mwa nchi hiyo kufuatia uharibifu wa bwawa hilo huku Urusi na Ukraine wakiendelea kushtumiana kuhusika na tukio hilo.
Mamlaka za Ukraine zimesema mafuriko hayo yatapelekea mamia kwa maelfu ya watu kukabiliwa na uhaba wa maji safi ya kunywa, kuharibu eneo kubwa la kilimo huku kukiwa na hatari ya kwamba takriban hekari 500,000 za mashamba zitashindwa kumwagiliwa na hivo kugeuka jangwa.
Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) limedhihirisha wasiwasi mkubwa juu ya athari za kijamii, kiuchumi na kimazingira kutokana na uharibifu wa bwawa hilo.
Ukraine yaomba msaada wa kimataifa
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy amesema hali ni mbaya huko Kherson na kwamba juhudi na msaada wa kimataifa vinahitajika. Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amelaani kitendo cha uharibifu wa bwawa hilo na kuahidi kuwa nchi yake itatuma misaada haraka.
Zelenskiy ameendelea kuwa mashirika ya kimataifa, hususan Shirika la Msalaba Mwekundu, wanatakiwa kujiunga mara moja na operesheni ya uokoaji na kusaidia watu katika eneo linalokaliwa na Urusi la Kherson, huku akisema kuwa Urusi inaendeleza mashambulizi licha ya hali hiyo ya dharura.
" Leo hii tahadhari kuu inaelekezwa kwa matukio ya kitendo cha ugaidi wa Urusi kwenye bwawa la kuzalisha umeme la Kakhovka. Maeneo mengi ya makazi katika eneo tunalodhibiti yamekumbwa na mafuriko. Ni maelfu ya nyumba. Tunaendelea kuwahamisha raia huku tukikabiliwa na mashambulizi ya makombora ya Urusi. Wanaendelea kushambulia bila kujali. Huu ni unyama."
Soma pia: Maelfu ya watu hatarini baada ya bwawa la Kakhovka kuripuliwa
Wakati hayo yakiarifiwa, mapambano yanaendelea. Naibu Waziri wa Ulinzi wa Ukraine Hanna Maliar amesema Jeshi lao limefanya mashambulizi makubwa na kupiga hatua huko Bakhmut, taarifa iliyokanushwa na Wizara ya Ulinzi ya Urusi iliyosema kuwa majaribio yote ya Ukraine huko Bakhmut yalizimwa.