Berlin: Kansela Gerhard Schröder amekua na mazungumzo pamoja na rais ...
11 Desemba 2003Matangazo
wa Poland Alexander Kwasniewski mjini Berlin.Mazungumzo yao yamesadif siku moja tuu kabla ya mkutano wa viongozi wa umoja wa ulaya mjini Brussels.Yamelengwa kusaka maridhiano kuhusu katiba mpya ya umoja wa ulaya.Poland na Hispania zinang'ang'ania mfumo wa sasa upigaji kura zikijivunia usemi wenye nguvu sawa na Ujerumani na Ufaransa.Rais Alexander Kwasniewski alitishia hapo awali kutumia kura ya turufu kuizuwia katiba mpya ya ulaya isiidhinishwe wakati wa mkutano wa viongozi mjini Brussels.Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Joschka Fischer kwa mara nyengine tena ametetea utaratibu ulioshauriwa ndani ya katiba mpya.Utaratibu huo uliopewa jina "wingi mara dufu" unazungumzia uamuzi wa nchi nyingi ambazo pia wakaazi wake wanapindukia asili mia 60 ya wakaazi jumla wa Ulaya.Waziri wa mambo ya nchi za nje Joschka Fischer amesema bora kusubiri kuliko kuharakisha kufikia makubaliano.Nasaha kama hiyo imetolewa pia na mwenyekiti wa kamisheni kuu ya Umoja wa Ulaya Romano Prodi.