Biden akutana kwa mara ya kwanza na viongozi ASEAN
13 Mei 2022Marekani imetangaza kutoa msaada wa fedha dola milioni 150 ili kusaidia nchi za Jumuiya ya Mataifa ya Kusini Mashariki (ASEAN) kuimarisha usalama wa baharini na miundombinu ya afya, huku viongozi wa ASEAN wakiwa na wasiwasi kuhusu upanuzi wa China katika eneo hilo.
Rais Joe Biden alianza mkutano wa kilele na viongozi wa ASEANkwa kuwaandalia chakula cha jioni viongozi wa jumuiya hiyo katika Ikulu ya White House siku ya Alhamis (Mei 12).
soma zaidi:Jeshi Myanmar lampinga ujumbe wa ASEAN
Huu ni mkutano wa kwanza kwa ASEAN unaofanyika siku mbili mjini Washington, wakati ambao Marekani inataka kuimarisha uhusiano na nchi za kusini mashariki mwa Asia kama sehemu ya mkakati wake wa Indo-Pacific katika kukabiliana na upanuzi wa China.
"Natumai mkutano huu unaweza kujenga kasi ya kurejea kwa uwepo wa Marekani katika kanda," Rais Joko Widodo wa Indonesia aliliambia kongamano la Baraza la Biashara la Marekani na Asia kabla ya kuelekea kwenye chakula cha jioni katika Ikulu ya Marekani.
Msaada wa fedha dola milioni 150 unajumuisha nini?
Marekani ilitoa dola milioni 60 kwa ajili ya kuimarisha kwa usalama wa baharini, ikijumuisha kutumwa kwa meli ya walinzi wa pwani na wafanyakazi wa kupambana na uhalifu baharini.
Maafisa wa Marekani walisema fedha hizo pia zitatumika kukabiliana na kile ambacho Marekani inakitaja kuwa uvuvi haramu unaofanywa na nchi ya China.
Dola milioni 40 katika hizo zitaelekezwa kwenye mipango ya nishati safi na dola milioni 6 ni kwa ajili ya maendeleo ya kidijitali katika eneo hilo.
Soma zaidi:Waziri Lwin wa Myanmar azuwiwa kushiriki mkutano wa ASEAN
Vile vile, Marekani ilisema inafanya kazi na sekta ya kibinafsi kutafuta kiasi cha fedha dola bilioni 2 nyengine.
Biden ana mipango ya kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi katika eneo hilo, kama vile uwekezaji wa miundombinu na Mfumo wa Kiuchumi wa Indo-Pasifiki (IPEF).
ASEAN ina wasiwasi gani kuhusu China?
China inadai kuwa bahari yote ya China Kusini inayopakana na wanachama wengine wanne wa ASEAN ambao ni Vietnam, Ufilipino, Brunei na Malaysia sehemu yake.
Wakati Marekani imeongeza ushirikiano na nchi nyingine za Indo-Pacific juu ya masuala ya usalama ili kukabiliana na China, wanachama wa ASEAN wameongeza hofu kutokana na Marekani kukawia katika mpango wake wa ukuaji wa uchumi katika eneo hilo tangu kujiondoa kwa mkataba wa biashara wa kikanda mwaka 2017.
"Marekani inapaswa kupitisha ajenda hai za biashara na uwekezaji na ASEAN, ambazo zitafaidisha Marekani kiuchumi na kimkakati," Waziri Mkuu wa Malaysia Ismail Sabri Yaakob alisema Alhamis.
China sio mwanachama wa ASEAN lakini ni mshirika wa kibiashara na Japan, Korea Kusini, Australia na New Zealand, ambazo ni wanachama wa ASEAN.
ASEAN ni nini?
ASEAN ni Jumuiya ya Mataifa ya Kusini Mashariki mwa Asia inayojumuisha wanachama 10: Brunei, Indonesia, Singapore, Thailand, Laos, Vietnam, Malaysia, Ufilipino, Myanmar na Cambonia, ikiwa na lengo la kuimarisha ushirikiano na ukuaji wa uchumi katika eneo la Asia na Pasifiki.
Ufilipino iliwakilishwa na katibu wake wa mashauri ya nchi za kigeni kwa vile nchi hiyo iko katika kipindi cha mpito, baada ya Ferdinand Marcos Jr. kuchaguliwa kama rais tarehe 9 Mei.
Soma zaidi:Australia na jumuiya ya ASEAN zaweka makubaliano mapya
Viongozi wanane wa ASEAN wanatarajiwa kushiriki katika mazungumzo siku ya Ijumaa, ambayo ni siku ya mwisho ya mkutano huo.
Kiongozi wa kijeshi wa Myanmar alizuiwa kuhudhuria mkutano wa mtandaoni wa mwaka jana mwezi Oktoba, na hakuwa na mwakilishi katikia mkutano huu.
Jenerali Min Aung Hlaing ametengwa kuhudhuria mikutano ya ASEAN kutokana na utawala wa kijeshina ghasia nchini humo.