Trump awatakia Xmas njema "wapuuzi" wa mrengo wa kushoto
25 Desemba 2024Rais wa Marekani Joe Biden na mrithi wake ajae, Donald Trump, walitoa ujumbe tofauti sana wa Krismasi Jumatano, huku Trump akisisitiza tena matamshi yake ya hivi karibuni kuhusu kuudhibiti Mfereji wa Panama, kuinunua Greenland, na kuiunganisha Canada na Marekani.
Biden alichapisha ujumbe mfupi wa msimu wa Krismasi uliolenga "wema na huruma," wakati Trump alituma machapisho zaidi ya thelathini kupitia mtandao wake wa Truth Social, akiwalenga moja kwa moja "wenda wazimu wa mrengo wa kushoto" na Waziri Mkuu wa Canada, Justin Trudeau, akilalamikia "kodi za juu mno za raia wa Canada."
Katika ujumbe wake mmoja, Trump alisema, "Krismasi Njema kwa Wenda wazimu wa Mrengo wa Kushoto, wanaojaribu kila mara kuzuia mfumo wetu wa mahakama na uchaguzi," akitumia mtindo wake wa kipekee wa herufi kubwa kiholela.
Trump alitumia siku ya Krismasi kulalamika kuhusu kile alichokiita mateso ya kisiasa dhidi yake, tofauti kabisa na ujumbe wa Biden wa "salamu za sikukuu kwa Wamarekani wote." Ushindi wa Trump katika uchaguzi wa Novemba ulijengwa juu ya mgawanyiko mkubwa wa kisiasa, ambao aliendelea kuutumia katika machapisho yake.
Soma pia: Orodha ya urathi wa Biden: Usitishaji vita Gaza, msaada kwa Ukraine, kampuni ya chuma ya Marekani
Miongoni mwa machapisho yake, Trump alijitangaza kuwa "Mzalendo wa Mwaka," akachapisha picha akitabasamu dhidi ya Barack Obama, na kusifu uteuzi wa baraza lake la mawaziri. Pia alieleza nia yake ya kuinunua Greenland na kulalamikia ada zinazolipwa na meli za Marekani kwa kutumia Mfereji wa Panama.
Trump alimuita Trudeau tena "gavana" wa Canada, akisema ikiwa nchi hiyo ingekuwa "Jimbo letu la 51, kodi zao zingepunguzwa kwa zaidi ya asilimia 60" na "biashara zao zingekua maradufu mara moja."
Soma pia: Trump, Biden wazungumzia mizozo ya Ukraine na Mashariki ya Kati
Alirudia vitisho vyake vya kudai udhibiti wa Marekani wa Mfereji wa Panama, akidai China ina ushawishi "haramu" juu ya mfereji huo na kwamba Washington inalipa "mabilioni ya dola kwa matengenezo" bila kuwa na usemi wowote.
Dakika chache baadaye, Trump alitangaza uteuzi wa mwanasiasa wa Florida, Kevin Marino Cabrera, kuwa balozi wake kwa Panama, akiitaja kuwa "nchi inayotutapeli kupitia Mfereji wa Panama kwa kiwango cha kushangaza."