Binadamu huchangia mabadiliko ya tabia nchi
27 Septemba 2013Taarifa hiyo imo katika ripoti iliyotolewa leo na jopo la wanasayansi wa mashirika ya nchi mbalimbali kuhusu mabadiliko ya tabia nchi, IPCC, na kuongeza kuwa viwango vya bahari vitaongezeka kati ya sentimita 26 hadi 82 ifikapo mwaka 2100. Aidha, ripoti hiyo imeonya kuhusu uwezekano wa kuwepo kwa mawimbi ya joto, mafuriko na ukame.
Wanaharakati wa mazingira pamoja na wanasayansi wamethibitisha katika ripoti hiyo iliyosubiriwa kwa muda mrefu na kuzinduliwa mjini Stockholm, Sweden, kwamba wanaamini kwa asilimia 95 binaadamu wamesababisha zaidi ya nusu ya ongezeko la joto katika kipindi cha miaka 60 iliyopita.
Ripoti yaandaliwa na wanasayansi 257
Ripoti hiyo yenye kurasa 2,000, ambayo imeandaliwa na wanasayansi 257, imeendelea kutabiri kwamba viwango vya joto vitaongezeka kwa nyuzijoto 0.3 hadi 4.8 katika kipimo cha Celcius.
Katika ripoti yake ya mwisho ya mwaka 2007, jopo hilo lilikadiria kuwa binaadamu wanachangia kwa asilimia 90 na kwamba viwango vya bahari vingeongezeka kati ya sentimita 18 hadi 59.
Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la mabadiliko ya tabia nchi, Christiana Figueres, amesema kuwa ripoti hiyo ni ishara kwamba dunia inapaswa kuzinduka.
Viongozi wengi duniani wametoa wito wa hatua kali kuchukuliwa katika kupunguza matumizi ya gesi inayochafua mazingira na kudhibiti kiwango cha nyuzijoto katika viwango vinavyowezekana.
Ban aizungumzia ripoti hiyo
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amesema ripoti hiyo inazitolea wito serikali kuuzingatia kwa makini mkataba wa Umoja wa Mataifa unaotaka mataifa mbalimbali duniani kupambana na ongezeko la joto duniani ifikapo mwaka 2015.
Amesema joto limeongezeka na sasa hakuna budi kulishughulikia suala hilo. Aidha, Ban amesema ataandaa mkutano wa mabadiliko ya tabia nchi mwezi Septemba, mwaka ujao wa 2014.
Kwa upande wake, mkuu wa shirika la utabiri wa hali ya hewa duniani, Michel Jarraud, amesema ripoti hiyo inasisitiza kwamba shughuli zinazofanywa na binaadamu kwa sasa, zina madhara makubwa kwa jamii, na sio tu jamii ya sasa, lakini jamii ya vizazi vingi vijavyo.
Jopo hilo tayari limeshazindua ripoti nne katika kipindi cha miaka 25 tangu liundwe. Utafiti wa ripoti hiyo ulijikita zaidi katika matumizi ya gesi inayochafua mazingira, hasa kutoka kwenye mkaa, petroli na gesi, ambavyo ndiyo uti wa mgongo wa usambazaji wa nishati kwa sasa.
Ripoti hiyo inazingatia mabadiliko ya vipimo vya hali ya hewa, kupanda kwa viwango vya maji ya bahari na kuyeyuka kwa maeneo ya barafu pamoja na ushawishi wa matukio hayo kwa binaadamu.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,RTRE
Mwandishi:Josephat Charo