1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSyria

Blinken asema raia wa Syria wanahitaji kulindwa

13 Desemba 2024

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken, amemwambia Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan kwamba raia wa Syria wanahitaji kulindwa baada ya waasi kuipindua serikali ya Rais Bashar al-Assad.

https://p.dw.com/p/4o5Nh
Rais wa Uturuki  Recep Tayyip Erdogan (kulia) amkaribisha waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken ( kushoto) kabla ya mkutano wao mjini Istanbul, Uturuki mnamo Januari 6, 2024
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan (kulia) na waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken ( kushoto)Picha: Mustafa Kamaci/Anadolu/picture alliance

Blinken alikutana jana jioni kwa zaidi ya saa moja na Rais Erdogan kwenye eneo la mapumziko katika uwanja wa ndege wa mji mkuu Ankara, muda mfupi baada ya kiongozi huyo wa Uturuki kumsindikiza waziri mkuu wa Hungary, Viktor Orban aliyekuwa anaondoka nchini humo baada ya ziara yake.

Wadau nchini Syria wahimizwa kuheshimu haki za binadamu

Katika taarifa, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Matthew Miller, amesema Blinken amesisitiza kuhusu umuhimu wa wadau wote nchiniSyriakuheshimu haki za binadamu, kuzingatia sheria ya kimataifa ya kibinadamu, na kuchukua hatua zote zinazowezekana kuwalinda raia, pamoja na watu kutoka kwa makundi ya walio wachache.

Uturuki yasema itajilinda dhidi ya makundi ya kigaidi

Kwa upande wake, Rais Erdogan amemwambia Blinken kwamba Uturuki itachukuwa hatua za kinga nchini Syriakwa usalama wake wa kitaifa dhidi ya makundi yote yanayochukuliwa kuwa ya kigaidi, na kuongeza kuwa Uturuki haitaruhusu udhaifu wowote katika mapambano yake dhidi ya kundi linalojiita dola la kiislamu IS.

Waasi walioko madarakani Syria wataka uhusiano mzuri na nchi zote

Waasi walioko madarakani kwasasa nchini Syria wamesema wanataka kuwa na uhusiano mzuri na nchi zote, huku wakiyashukuru mataifa kadhaa kwa kudumisha shughuli katika balozi zao huko Damascus.

Bunge, Katiba vyasitishwa kwa miezi mitatu Syria

Katika taarifa iliyochapishwa kwenye mitandao yake ya kijamii, Idara ya Masuala ya Kisiasa inayosimamiwa na waasi hao, imesema wanatumaini kujenga uhusiano mzuri na nchi zote zinazoheshimu mapenzi ya watu wa Syria pamoja na uhuru na umoja wa nchi hiyo.

Wapiganaji wa upinzani nchini Syria washerehekea baada ya kupinduliwa kwa serikali ya Syria mjini Damascus mnamo Desemba 8,2024
Wapiganaji wa upinzani nchini SyriaPicha: Omar Sanadiki/AP Photo/picture alliance

Waasi hao pia walipishukuru Misri, Iraq, Italia na mataifa kadhaa ya Ghuba kwa kuanzisha tena shughuli katika balozi zao mjini Damascus.

Pia walipongeza ahadi za Qatar na Uturuki za kufungua tena balozi zao hivi karibuni.

Hapo jana, Jamhuri ya Czech pia ilisema inataka kufungua tena Ubalozi wake nchini humo haraka iwezekanavyo.

Jordan kuandaa mazungumzo kuhusu Syria

Jordan imesema itaandaa mazungumzo ya wanadiplomasia wakuu kujadili hali nchini Syria baada ya kupinduliwa kwa serikali ya al-Assad.

Kundi la G7 lasema liko tayari kuisaidia Syria

Mawaziri wa mambo ya nje wa Jordan, Saudi Arabia, Iraq, Lebanon, Misri, Umoja wa Falme za Kiarabu, Qatar na Bahrain pamoja na mkuu wa Umoja wa nchi za Kiarabu, watakutana kesho Jumamosi katika mji wa Aqaba nchini Jordan. Haya ni kwa mujibu wa wizara ya mambo ya nje ya nchi hiyo.

Zaidi ya watu milioni moja wapoteza makazi Syria

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuratibu Masuala ya Kiutu OCHA, limesema jana kwamba zaidi ya watu milioni moja, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, wamekimbia makazi yao nchini Syriatangu waasi walipoanzisha mashambulizi ya kumuondoa madarakani Rais Bashar al-Assad.