Blinken awasili Israel huku vita vya Gaza vikiendelea
12 Oktoba 2023Jeshi la Israel limeendeleza mashambulizi ya maelfu ya makombora huko Gaza baada ya wanamgambo wa Hamas kuwauwa Waisraeli wapatao 1,200 wengi wao wakiwa ni raia na kuwachukua mateka watu wapatao 150.
Zaidi ya Wapalestina 1,200 wamepoteza maisha pia huko Gaza huku Israel ikiharibu kabisa maelfu ya majengo tangu Hamas ilipoanzisha mashambulizi ya umwagaji damu ambayo hayajawahi kushuhudiwa katika historia ya Israel.
Soma pia: Mashambulizi Israel, Gaza yaingia siku ya sita
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amelihutubia taifa jana usiku na kurejelea azma yake ya kuwalipiza kisasi Hamas ambao amewafananisha na kundi la kigaidi linalojiita Dola la Kiislamu IS na kuahidi kuwa "atawaangamiza."
"Tunapigana kwa nguvu zetu zote, katika pande zote. Tumekuwa tukishambulia. Na kila mwanachama wa Hamas ni maiti mtarajiwa."
Hamas inazingatiwa na Marekani, Umoja wa Ulaya ikiwemo Ujerumani na baadhi ya mataifa mengine kuwa kundi la kigaidi.
Mshikamano wa Marekani kwa Israel
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken amewasili hii leo mjini Tel Aviv kama sehemu ya ziara ya Mashariki ya Kati ili kuonyesha mshikamano wa Washington kwa Israel baada ya mashambulizi ya wapiganaji wa Hamas.
Blinken atajaribu pia kusaidia mchakato wa kuachiliwa kwa watu waliotekwa na Hamas, ambao baadhi yao ni Wamarekani. Mwanadiplomasia huyo wa Marekani atajaribu pia kupiga jeki mazungumzo kati ya Israel na Misri juu ya kuwepo njia salama watakayotumia raia wa Gaza wanaokabiliwa na mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Israel.
Soma pia: Israel yaushambulia Ukanda wa Gaza katika siku ya 5 ya vita vyake na Hamas
Rais wa Marekani Joe Biden ambaye ameiunga mkono Israel na kuanza kutuma msaada wa kijeshi amesisitiza jana kwamba licha ya "hasira na mfadhaiko" walionao, Israel inapaswa kuendesha mashambulizi yake kwa kuzingatia sheria za vita.
Hofu imekuwa ikiongezeka kwa wakazi milioni 2.4 wa Gaza ambao sasa wanakabiliwa na vita vya tano katika kipindi cha miaka 15 katika eneo hilo lililozingirwa kwa muda mrefu, ambalo pia limeshuhudia Israel ikikata huduma ya maji, umeme na kuzuia kuwasilishwa kwa chakula.
Waziri wa Nishati wa Israel Israel Katz ameapa leo Alhamisi kwamba kuzingirwa kwa Gaza kutaendelea hadi pale mateka watakapoachiwa huru. Nalo kundi la Hamas limetishia kuwaua mateka hao iwapo Israel itashambulia maeneo ya raia huko Gaza bila kutoa taarifa mapema, jambo linalozidisha hasira na hofu huko Israel.
Vita vya Israel vinavyopamba moto eneo la kusini vinatatizwa zaidi na tishio kutoka kaskazini, ambapo kundi la Hezbollah lenye makao yake makuu nchini Lebanon na linaloungwa mkono na Iran limekuwa pia likiishambulia Israel.
Umoja wa Mataifa walaani ghasia za vita hivyo
Makumi ya wataalam huru wa Umoja wa Mataifa wamelaani leo hii "uhalifu wa kutisha" wa Hamas lakini wakasema mashambulizi ya Israel katika Ukanda wa Gaza "ni sawa na adhabu ya jumla".
Wataalam hao wamesema na hapa nawanukuu : " Hakuna uhalali wa ghasia zinazolenga raia kiholela na wasio na hatia, iwe zinaendeshwa na Hamas au vikosi vya Israel. Jambo hili ni marufuku kabisa kwa mujibu wa sheria ya kimataifa na ni sawa na uhalifu wa kivita."
Soma pia: Papa Francis airai Hamas kuwaachia mateka, aeleza wasiwas mzingiro Gaza
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametaja kuwa na wasiwasi kuhusu "matukio ya kutisha na ya mara kwa mara ya ghasia" , huku akihimiza kuachiliwa kwa mateka wote na kuondolewa kwa mzingiro wa Gaza. Guterres amesisitiza kwamba "raia ni lazima walindwe wakati wote".