Blinken kufanya ziara ya tano Mashariki ya Kati
3 Februari 2024Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken kwa mara nyingine tena anatarajiwa kuhudhuria mazungumzo ya mgogoro wa Mashariki ya Kati.
Kwa mujibu wa msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Matthew Miller kuanzia Jumamosi hii hadi Februari 8, Blinken atazuru nchi za Saudi Arabia, Misri, Qatar, Israel na Ukingo wa Magharibi.
Safari ya hiyo tano ya Blinken kuelekea Mashariki ya Kati tangu kuanza kwa vita vya Gaza karibu miezi minne iliyopita, inafuatia jeshi la Marekani kufanya mashambulizi katika maeneo lengwa ya Iraq na Syria.
Wakati wa ziara yake, Blinken ataendeleza juhudi za kidiplomasia za kufikia makubaliano ya usitishaji mpya wa mapigano katika vita vya Gaza, baina ya Israel na Hamas pamoja na kuachiwa huru mateka. Usitishaji huo pia utaruhusu usambazaji wa misaada ya kiutu kwa Wapalestina.