Bunge la Duma lajiandaa kuuidhisha mkataba wa START,Urusi
24 Desemba 2010Rais wa Urusi, Dmitry Medvedev, amempongeza hii leo mwenzake wa Marekani, Barack Obama, na kumuelezea kuwa kiongozi anayezitimiza ahadi zake. Kauli hizo zimetolewa baada ya Marekani kuuidhinisha siku ya Jumatano mkataba wa START. Kulingana na makubaliano hayo, Urusi na Marekani zitalazimika kuipunguza idadi yao makombora yao ya nuklia hadi 1500 kutokea 2200.
Awamu tatu za kura
Bunge hilo la Duma linajiandaa hii leo kuupigia kura mkataba huo katika awamu ya kwanza kati ya tatu, katika kikao chake cha mwisho cha mwaka huu. Wabunge wanatazamiwa kuyapitisha maazimio yao ambayo hayataubadili mkataba wenyewe ila kuuwasilisha mtazamo wake unaoupinga mpango mpya wa Marekani wa kuweka makombora ya kujihami barani Ulaya. Hata hivyo, viongozi hao bado hawajaipokea rasimu hiyo iliyoidhinishwa na bunge la Senate la Marekani, kama anavyoelezea Waziri wa Mambo ya kigeni wa Urusi,Sergei Lavrov,kuwa''Wizara ya mambo ya kigeni imewafahamisha wabunge kuhusu mipango hiyo ya kuiidhinsiha rasimu hiyo. Hatua hiyo ni muhimu kwani kilichomo ndicho kitakachotuamulia kauli yetu. Ijapokuwa tunafahamu kuwa Marekani imeshaiidhinisha rasimu hiyo, bado hatujaipokea hati rasmi. Hata hivyo, tuko tayari kuiidhinisha pindi kikao cha Duma kitakapoitishwa,''alifafanua.
Vipengee tete
Baadhi yao wanatiwa wasiwasi na kilichomo kwenye rasimu yenyewe.Kwa upande wao, wabunge wa Marekani wanafahamu kuwa baadhi ya vipengee vilivyofanyiwa mabadiliko, zaidi vinaihusu nchi yao. Mkataba huo mpya uliidhinishwa siku ya Jumatano, baada ya kipindi kirefu cha mivutano katika bunge la Senate la Marekani.Pindi baada ya uamuzi huo kufikiwa,Rais Obama aliipongeza,''Mkataba huo ulio na uzito mkubwa kwenye masuala ya kuyapunguza matumizi ya nyuklia katika kipindi cha yapata miongo miwili. Azma yake ni kutuhakikishia usalama vilevile kuipunguza idadi ya zana zetu na za Urusi za nuklia,'alisisitiza.
Vichwa 800
Kulingana na mkataba huo mpya Urusi na Marekani zinalazimika kuipunguza idadi yao kamili ya vichwa vya nuklia hadi 1500. Hii ina maana kuwa kila nchi itakuwa na kiasi ya makombora 800 pekee.
Kwa upande mmoja mkataba huo unaifariji Urusi ambayo itakuwa na idadi sawa ya zana za nuklia na Marekani. Kwa upande wa pili, Marekani inaamini kuwa hati hiyo itauimarisha uhusiano kati ya mataifa hayo mawili na pia itaziongezea msukumo harakati za jamii ya kimataifa za kuizuwia Iran kuendelea na mpango wake wa nuklia unaozua utata.
Mwandishi:Mwadzaya,Thelma-AFPE/DPAE
Mhariri: Miraji Othman