1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Bunge la Israel lajadili muswada tata wa mageuzi ya mahakama

Sylvia Mwehozi
21 Februari 2023

Rais wa Israel Isaac Herzog ametoa wito kwa muungano tawala wa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kutafuta maridhiano baada ya wabunge kuupigia kura muswada wa marekebisho ya mahakama uliojaa utata.

https://p.dw.com/p/4NndJ
Israel Knesset Benjamin Netanyahu
Picha: Maya Alleruzzo/AP Photo/picture alliance

Bunge la Israel limechukua hatua katika uidhinishaji wa mageuzi ya mahakama yaliyo na utata licha ya wiki kadhaa za maandamano ya umma dhidi ya sheria hiyo ambayo wakosoaji wanaitizama kama kitisho kwa demokrasia. Wabunge walipiga kura 63 dhidi ya 47 za kuunga mkono muswada huo wa mageuzi wakati ulipowasilishwa bungeni kwa mara ya kwanza. Muswada huo bado unahitaji kuwasilishwa mara mbili bungeni kabla ya kupitishwa kuwa sheria. 

Ushindi huo wa Jumatatu, unamaanisha kuwa bunge la Israel linalojulikana kama Knesset limeidhinisha hatua zinazoupatia muungano tawala udhibiti zaidi juu ya uteuzi wa majaji na kuzuia uwezo wa mahakama ya juu wa kupitia "sheria za msingi" ambazo zina jukumu la kikatiba nchini Israel ambayo haina katiba rasmi.Serikali mpya ya Netanyahu kuapishwa Israel

Rais wa Israel Isaac Herzog, ambaye amekuwa akijaribu kuitisha mazungumzo juu ya mageuzi hayo ambayo yataimarisha mamlaka ya wanasiasa dhidi ya mahakama, ameonya juu ya muswada huo kuleta mgawanyiko wa kitaifa. Rais Herzog ambaye mamlaka yake kwa kiasi kikubwa si ya kiutendaji ametaka kufanyike mazungumzo baada ya kura ya jana ili kufikia mwafaka unaokubalika wa kuliondoa taifa hilo katika kipindi kigumu.

Protest gegen Justizreformen in Israel
Maandamano ya kupinga muswada wa marekebisho ya mahakama mjini JerusalemPicha: Ohad Zwigenberg/AP/picture alliance

Marekebisho hayo yana umuhimu mkubwa kwa utawala wa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, ambao unaundwa na vyama vya Orthodox na vyama vya mrengo mkali ambavyo vilichukua madaraka mwishoni mwa Desemba. Kuelekea kura ya Jumatatu usiku maelfu ya Waisraeli waliandamana nje ya bunge, hayo yakiwa ni maandamano ya pili makubwa mjini Jerusalem katika wiki za hivi karibuni. Waziri Mkuu Netanyahu amewashutumu wakosoaji wake akisema kuwa;

"Katika demokrasia wananchi wanapiga kura katika uchaguzi na wawakilishi wa wananchi wanapiga kura hapa Knesset na hiyo inaitwa demokrasia, lakini kwa bahati mbaya viongozi wa maandamano wanaikanyaga demokrasia, hawakubali matokeo ya uchaguzi, hawakubali uamuzi wa wengi."

Baada ya zaidi ya saa saba za mjadala ulioendelea baada ya saa sita usiku, Netanyahu na washirika wake walipitisha vifungu viwili katika muswada wa marekebishoyanayopendekezwa ambayo yanalenga kudhoofisha mamlaka ya kimahakama na kulipatia mamlaka zaidi bunge la muungano unaotawala.

Kulingana na utafiti uliochapishwa siku ya Jumanne na Taasisi ya Demokrasia ya Israel unaonyesha kuwa asilimia 66 ya waliohojiwa wanafikiri mahakama ya juu inapaswa kuwa na mamlaka ya kufuta sheria zisizoendana na katiba na asilimia 63 wanafikiri mfumo wa sasa wa kuchagua majaji unaojumuisha wanasiasa, majaji na mawakili unapaswa kuendelea kutumika.

Kiongozi wa upinzani Yair Lapid amewakosoa wabunge baada ya kura ya jana akisema kwamba "historia itawahukumu kwa kuishambulia demokrasia, uchumi, usalama na kuvuruga umoja wa wananchi".