Ujerumani yaifanyia mageuzi sheria ya uraia
20 Januari 2024Serikali imetoa hoja kuwa mpango huo utasaidia ujumuishwaji wa wahamiaji na kuwavutia wafanyakazi wenye ujuzi kufanya kazi Ujerumani.
Bunge la Ujerumani lilipiga kura 382 dhidi ya 234 kwa ajili ya kuupitisha mpango huo uliowasilishwa na muungano wa vyama vinavyounda serikali inayoongozwa na Kansela Olaf Scholz. Wabunge 23 hawakupiga kura.
Sheria hiyo mpya itawafanya watu kuwa na sifa ya kuomba uraia wa Ujerumani baada ya miaka mitano au miaka mitatu ikiwa atakidhi viwango maalumu. Watoto waliozaliwa Ujerumani watakuwa raia moja kwa moja ikiwa mzazi mmoja amekuwa mkaazi kwa miaka mitano, tofauti na minane ya hapo awali.
Soma zaidi: Ujerumani yakubali kulegeza sheria za uraia kwa wahamiaji
Vikwazo vya kuwa na uraia pacha navyo vitaondolewa. Kabla ya mageuzi haya watu wengi kutoka nchi zilizo nje ya Umoja wa Ulaya na Uswisi, walitakiwa kuukana uraia wa nchi zao ili kupata Uraia wa Ujerumani.
Asilimia 14 ya wakaazi hawana uraia wa Ujerumani
Serikali inasema kuwa asilimia 14 ya idadi ya watu ambayo ni zaidi ya watu milioni 12 waishio Ujerumani hawana uraia wa Ujerumani na kwamba milioni 5.3 kati ya hao wameishi nchini humo kwa takribani muongo mmoja.
Mwaka 2022 takribani watu 168,500 walipewa uraia wa Ujerumani idadi hiyo ikiwa ni kubwa zaidi tangu mwaka 2002. Idadi hiyo ilichochewa na ongezeko la raia wa Syria waliopata uraia kwa kuasiliwa katika muongo mmoja uliopita.
Hata hivyo sheria ya sasa inaainisha kuwa, watu wanaopata uraia kwa kuasiliwa wanapaswa kuwa na uwezo wa kujihudumia ingawa kuna msamaha kwa watu waliofika Ujerumani magharibi kama wafanyakazi wageni hadi kufikia mwaka 1974, na wale waliokuja kufanyakazi kwa iliyokuwa Ujerumani Mashariki.
Mageuzi ya sheria hiyo ni moja ya mabadiliko ya kijamii ambayo serikali ya muungano wa vyama vinavyundwa na serikali inayoongozwa na kansela Scholz ilikubaliana kuyafanya wakati ilipoingia madarakani mwaka 2021.