Burundi: Buyoya apewa kifungo cha maisha kwa kumuuwa Ndadaye
21 Oktoba 2020Mahakama hiyo imesema katika tangazo la hukumu hiyo dhidi ya Meja Pierre Buyoya, kuwa kiongozi huyo wa zamani amepewa kifungo cha maisha jela kutokana na mchango wake katika mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 1993 dhidi ya Rais Melchior Ndadaye, ambaye alikuwa amekaa madarakani kwa miezi michache tu baada ya kumshinda Buyoya katika uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia kufanyika nchini Burundi, tangu nchi hiyo ilipopata uhuru wake kutoka ukoloni wa Kibelgiji mwaka 1962.
Soma zaidi: Burundi yawakamata maafisa wa kijeshi kwa mauaji ya Ndadaye mwaka 1993
Hukumu hiyo iliyotangazwa kwenye mkesha wa kumbukumbu ya miaka 27 tangu kuuawa Ndadaye, imewahusisha pia maafisa wengine waandamizi wa zamani 18, wakiwemo wawili waliokuwa makamu wa rais, Bernard Busokoza na Alphonse Marie Kadege.
Kama ilivyo kwa Buyoya, Busokoza na Kadege wote wanaishi uhamishoni, na wamehukumiwa bila kufika mahakamani.
Buyoya bado anaheshimiwa Afrika
Kwa wakati huu, Pierre Buyoya ni mjumbe maalumu wa Umoja wa Afrika nchini Mali na katika ukanda wa Sahel, licha ya kuwekewa na nchi yake waranti wa kimataifa wa kukamatwa, tangu Novemba 2018.
Mmoja wa watu hao waliohukumiwa aliyezungumza na shirika la habari la AFP kwa masharti ya kutotajwa jina, amesema hukumu hiyo iliyotolewa bila ya wao kuwepo, ilikuwa ni kama mchezo wa kuigiza.
Soma zaidi: Burundi yatoa waranti wa kumkamata Buyoya
Melchior Ndadaye, rais wa kwanza wa Burundi aliyechaguliwa kidemokrasia, akiwa pia rais wa kwanza kutoka jamii ya Wahutu, aliuawa pamoja na mawaziri wake kadhaa katika mashambulizi yaliyofanywa na wanajeshi kutoka jamii ya Kitutsi, miezi minne tu baada ya kuingia madarakani, kufuatia ushindi wa kishindo alioupata dhidi ya Buyoya.
Wengi waangamia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe
Mauaji hayo yaliitumbukiza Burundi katika mgogoro mkubwa wa umwagaji damu, uliowahusisha wanajeshi wa kitutsi, na wanamgambo wa vuguvugu lililoongozwa na chama cha FRODEBU cha Melchior Ndadaye kilichodhibitiwa na Wahutu. Mgogoro huo uliodumu kwa miaka 10 uliangamiza maisha ya watu wapatao 300,000.
Mrithi wa Rais Melchior Ndadaye, Cyprien Ntaryamira aliuawa pia miezi michache baada ya kuchukuwa madaraka, alipokuwa akisafiri katika ndege moja na rais wa zamani wa Rwanda Juvenal Habyarimana, ambayo ilidunguliwa katika anga la mji mkuu wa Rwanda Kigali Tarehe 6 Aprili 1994, na kuwauwa wote waliokuwemo.
Tukio hilo pia lilifuatiwa na umwagaji mkubwa wa damu nchini Rwanda, uliogeuka mauaji ya kuangamiza dhidi ya watu wa jamii ya watutsi, ambapo, watu takribani milioni moja walipoteza maisha. Meja Pierre Buyoya mwenyewe hajatamka lolote baada ya hukumu hiyo.
afpe, rtre