Chama cha CSU chashinda uchaguzi Bavaria
16 Septemba 2013Chama cha CDU ndicho kinachoiongoza serikali ya mseto ya Ujerumani. Hapakutokea kadhia yoyote ya kushangaza katika uchaguzi wa jimbo la Bavaria-jimbo kubwa kabisa la kusini mwa Ujerumani. Matokeo ya uchaguzi yalikuwa kama jinsi yalivyotabiria katika kura za maoni.
CSU yasahihisha makosa yake
Chama cha CSU safari hii kimeweza kuyasahihisha makosa yaliyofanywa mnamo mwaka wa 2008.Katika uchaguzi wa mwaka huo chama cha CSU kiliteleza kwa kiwango kilichozingatiwa kuwa cha kihistoria kiasi cha kulazimika kuyasikia maoni ya wananchi yaliyotolewaa kwa njia ya kupiga kura.Chama cha CSU kiliuhitaji msaada wa chama ndugu cha Waliberali,FDP ili kuweza kupata wingi wa uhakika bungeni.
Lakini katika uchaguzi wa safari hii chama cha CSU kilipata asilimia 49 ya kura. Mwenyekiti wa chama hicho Horst Seehofer ambaye pia ni Waziri mkuu wa jimbo la Bavaria amesema yafuatayo juu ya ushindi wa chama chake katika uchaguzi. "Huo ni ushindi mzuri sana. Chama cha CSU ni cha umma na kimefungamana na wananchi wa Bavaria katika mizizi. Nusu ya wananchi wa jimbo hilo walitupigia kura."
Hata hivyo ushindi huo unaweza kuwa wa mashaka kwa Kansela Angela Merkel.Chama cha Waliberali, FDP hakikuweza kufikia asilimia tano ya kura, na hivyo kimeshindwa kuingia bungeni.
Chama hicho kiliambulia asilimia tatu tu za kura. Ni maoni ya wachambuzi kwamba katika uchaguzi mkuu wiki ijayo wapiga kura wafuasi wa chama cha bibi Merkel cha CDU huenda wakakipa chama hicho kura za huruma. Hatua hiyo itapunguza hesabu ya kura za chama cha Kansela Merkel,CDU
Chama cha FDP tegemeo la CDU
Chama cha Bibi Merkel cha CDU kinakihitaji chama cha FDP ili kiweze kuendelea kuwamo katika uongozi wa serikali. Lakini chama ndugu cha FDP kitapaswa kupata zaidi ya asilimia tano ya kura katika uchaguzi mkuu wa tarehe 22 Kwa mujibu wa kura za maoni
Kansela Merkel yaupo mbele ya mshindani wake mkuu Peer Steinbrück anaegombea ukansela kwa tiketi ya chama kikuu cha upinzani cha Social Demokratik.
Lakini siku za hivi karibuni zimeonyesha kwamba Steinbrück ameweza kulipunguza pengo kidogo. Katika uchaguzi wa jimbo la Bavaria chama cha bwana Steinbrück kilipata asilimia zaidi ya asilimia 20. Hayo siyo matokeo ya kusisimua kwa chama cha SPD lakini kwa, kuzingatia kwamba jimbo la Bavaria ni ngome madhubuti ya chama cha CSU, matokeo hayo ni ushindi kwa chama cha SPD.
Mwandishi: Wagener Volker
Tafsiri: Mtullya Abdu.
Mhariri: Josephat Charo