1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Democrats kumpitisha Biden kuwa mgombea urais Marekani

17 Agosti 2020

Chama cha Democratic nchini Marekani kinaanza mkutano wake mkuu, ambao ndio utakaompitisha rasmi Joe Biden kuwa mgombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa Novemba mwaka huu.

https://p.dw.com/p/3h4j9
Joe Biden und Kamala Harris USA Wahlen 2020
Picha: picture-alliance/dpa/C. Kaster

Mkutano huu unafanyika kwa njia ya mtandao kwa sababu ya janga la virusi vya korona. Ukiwa mkutano wa kwanza mkubwa wa uteuzi kufanyika kwenye zama hizi za korona, kongamano hili linaloanza leo limelazimika kuhamia zaidi kwenye njia za dijitali na hivyo kulinyima ile hamasa ya umma kukusanyika pamoja kwenye ukumbi mkubwa wenye kila aina ya shamrashamra.

Hotuba za Joe Biden, mgombea mwenza wake Kamala Harris, na vigogo wengine wa chama cha Democratic zitarushwa kuanzia saa 7:00 hadi saa 9:00 mchana kila siku kuanzia leo hadi Agosti 20. Wazungumzaji wa leo ni pamoja na mke wa rais wa zamani, Barack Obama, Michelle Obama, Seneta Bernie Sanders na magavana Andrew Cuomo na Gretchen Whitmer.

Wamarekani watakiwa kumshinda Trump

Akizungumza hapo jana, Sanders ambaye aliwania na kushindwa tena kwenye kura za mchujo za kiti cha urais, alisema kwamba ni jambo la lazima kwa Wamarekani kumshinda Donald Trump kwenye uchaguzi wa mwaka huu.

Kwa mujibu wa mtandao wa chama hicho, hotuba za jioni zitatolewa na watu waliojitolea kukabiliana na matatizo yanayoikumba jamii "kama vile janga la COVID-19, ambalo linaendelea kulikabili taifa hili, huku mamilioni ya watu wakipoteza ajira zao, na Marekani ikipambana na dhuluma kubwa ya ubaguzi.”

USA - Bill Clinton und Barack Obama
Marais wa zamani wa Marekani, Barack Obama na Bill Clinton Picha: picture-alliance/CPA Media Co. Ltd

Katika orodha wa wazungumzaji wamo pia marais wa zamani Barack Obama na Bill Clinton na wanamuziki Billie Eilish na John Legend watakaotumbuiza.

Kamala Harris, mwenye umri wa miaka 55, anatazamiwa kuweka historia ya kuwa mwanamke wa kwanza mwenye asili ya Afrika kukubali uteuzi wa kuwa mgombea mwenza siku ya Jumatano. Mwanasiasa huyo ambaye ana mchanganyiko wa Kiafrika na Kiasia, atakuwa pia Mmarekani wa kwanza mwenye asili ya Asia kuchaguliwa kwa nafasi hiyo.

Ratiba ya uteuzi

Ratiba inaonesha kuwa uteuzi rasmi wa Biden utafanyika siku ya Alkhamis, ambapo kwenye hotuba yake anatazamiwa kuzungumzia dira yake ya kuiunganisha Marekani na kuitowa kwenye machafuko na mzozo wa sasa, kwa mujibu wa chama chake. Biden, mwenye umri wa miaka 77, atalihutubia taifa akiwa jimbo la kwao la Delaware, kama sehemu ya hatua za hadhari dhidi ya maambukizo ya virusi vya korona.

Makamu huyo wa rais wa zamani anaingia kwenye mkutano huu akiwa anaongoza kwenye uchunguzi wa maoni mbele ya Trump, huku uteuzi wake wa Kamala Harris kama mgombea mwenza ukimuongezea matumaini ya kupata kura za makundi maalum kama vile wanawake, Waafrika na Waasia. Mkutano mkuu wa mahasimu wao wa Republican utafanyika mnamo tarehe 24 Agosti.

(DPA, AFP)