1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama cha AfD chashinda uchaguzi Thuringia

2 Septemba 2024

Kwa mara ya kwanza katika historia yake, chama cha mrengo wa kulia cha Mbadala kwa Ujerumani AfD kimepata ushindi katika uchaguzi wa jimbo.

https://p.dw.com/p/4kA4c
Mwenyekiti wa chama cha AfD katika jimbo la Thuringia. Björn Höcke
Mwenyekiti wa chama cha AfD katika jimbo la Thuringia. Björn HöckePicha: Bodo Schackow/dpa/picture alliance

Chama cha Mbadala kwaUjerumani, AfD, kimeibuka na nguvu katika jimbo la mashariki la Thuringia kwa kushinda asilimia kiasi 33 ya kura. Katika jimbo jirani la Saxony chama hicho kimeshika nafasi ya pili na asilimia kiasi 30 ya kura, nyuma ya chama kinachotawala cha Christian Democratic Union, CDU.

Matokeo hayo yamekuwa yakisubiriwa kwa wasiwasi huku mashirika ya upelelezi wa ndani katika majimbo yote mawili yakikiorodhesha chama cha AfD kama cha mrengo mkali wa kulia.

Mwenyekiti wa chama cha AfD katika jmbo la Thuringia, Björn Höcke, anachukuliwa kuwa kiongozi mwenye msimamo mkali zaidi katika chama chake. Mara kwa mara ametumia kauli za kinazi na alitiwa hatiani mara mbili mahakamani mwaka huu kwa kutumia kauli ya kinazi iliyopigwa marufuku katika mikutano yake ya kampeni.

Soma pia: Wapiga kura katika majimbo mawili ya mashariki mwa Ujerumani wapiga kura

Hali ilikuwa ya sherehe na shangwe miongoni mwa wafuasi wa chama cha AfD kufuatia ushindi huo ambao wachambuzi wameueleza kuwa ni 'tetemeko kubwa la ardhi' katika siasa. Kwao wao, shujaa ni Bjoern Hoecke, mwalimu wa zamani wa historia aliyegombea katika uchaguzi wa jimbo la Thuringia na kukipa ushindi mkubwa kabisa chama cha AfD ambao haujawahi kushuhudiwa.

"Alikuwa lazima ashinde," alisema mfuasi wa chama cha AfD, Patrick Teichman, mwenye umri wa miaka 32, macho yake yakiwa yamemng'aa kwa furaha, kufuatia kupanda kwa chama hicho ambacho kimeapa kuwarejesha kwao wahamiaji wasio halali.

Wachambuzi wengi Wajerumani wana wasiwasi mkubwa kuhusu kuimarika kwa chama cha AfD katika muongo mmoja uliopita kutoka kwa kundi ambalo halikuwa maarufu hadi kufikia vuguvugu la kizalendo linalopinga uhamiaji.