Chanjo zaidi ya 11,000 kupelekwa Guinea kukabiliana na ebola
19 Februari 2021Kulingana na mkurugenzi wa shirika hilo kanda ya Afrika Matshidiso Moeti, chanjo hizo 11,000 zinatayarishwa mjini Geneva na zinatarajiwa kufikishwa Guinea mwishoni mwa Juma. Chanjo nyengine za ziada 8,600 zitatolewa Marekani huku akitangaza kuwa mchakato wa kuwachanja watu unatarajiwa kuanza siku ya Jumatatu.
Moeti, amesema wataalamu 30 wa kutoa chanjo wapo tayari kuanza kazi hiyo wakati chanjo zitakapowasili nchini humo. Shirika hilo la Afya duniani WHO limezitolea mwito mataifa mengine sita ya Afrika kuwa makini kuzuwia maambukizi ya ugonjwa wa ebola nchini mwao baada ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na Guinea kurekodi visa kadhaa katika wiki za hivi karibuni.
Janga la ebola nchini Guinea lilitangazwa baada ya mkutano siku ya Jumapili ikiwa ni chini ya mwezi mmoja baada ya maafisa wa usalama kugundua wagonjwa kadhaa walioonesha dalili za kuharisha, kutapika, na kuvuja damu. Wagonjwa hao walishiriki maziko ya muuguzi mmoja aliyefariki dunia mwishoni mwa mwezi Januari na kuzikwa tarehe mosi Februari, hii ikiwa ni kwa mujibu wa Wizara ya afya nchini humo.
Maziko ya kitamaduni ambapo watu humuosha na kumshika maiti ndio moja ya sababu ya kusambaa kwa ugonjwa wa ebola, ugonjwa ulioingia kwa wanaadamu baada ya kutoka kwa wanyama kama vile popo na kisha kusambaa haraka kwa binaadamu kupitia majimaji ya mwilini kama vile majasho na machozi.
Huenda Maataifa jirani yakawa katika hatari ya kukabiliwa na ugonjwa wa Ebola
Hapo jana WHO ilisema Guinea imerekodi visa vitatu vilivyothibitishwa vya ebola ikiwemo kifo cha mtu mmoja. Maafisa wa Usalama hata hivyo wana matumaini ya kuutokomeza ugonjwa huo katika mataifa ya Afrika Magharibi iliojikuta ikipambana na janga baya zaidi la ugonjwa huo mwaka 2014 hadi 2016 na kusababisha vifo vya watu 11,300 wengi kutoka Guinea, Liberia na Sierra Leone.
Huku hayo yakiarifiwa katika nchi hizo jirani za Liberia na Sierra Leone tayari zinapambana na visa vinavyoshukiwa kuwa vya ebola katika mipaka yake.
Waziri wa Afya wa Liberia, Dk. Wilhelmina Jallah amesema wafanyakazi wa afya wanamfanyia vipimo mwanamke aliyeingia nchini humo kutoka Guinea aliyeonyesha dalili za ebola. Mwanamke huyo yuko karantini na anasubiri majibu ya vipimo vyake. Nchini Sierra Leone mapema wiki hii mwanamume mmoja pia alipatikana akiwa na dalili za ugonjwa huo yuko pia karantini amefanyiwa vipimo na anasubiria majibu yake.
Umoja wa Mataifa kwa upande wake umetangaza kutoa msaada wa fedha wa dola milioni 15 kutoka katika mfuko wake wa dharura ili kuisaidia Guinea na Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo kupambana na janga hilo.
Kongo ilitangaza kisa chake cha kwanza cha ebola tarahe 8 Februari Mashariki mwa nchi hiyo ikiwa ni kisa cha kwanza kutokea tangu mwaka 2020. Chanjo elfu 8 zimepelekwa huko na mchakato wa kuwachanja watu umeanza siku ya Jumatatu katika mji wa Butembo kwa watu walio na magonjwa nyemelezi na waleo walio katika hatari kama wazee.
Chanzo: ap