1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Conceicao aipa ushindi Portugal kwa bao la dakika za mwisho

19 Juni 2024

Francisco Conceicao alifunga bao la ushindi dakika za lala salama wakati Ureno ilipoibwaga Jamhuri ya Czech kwa mabao 2-1 katika mechi yao ya kwanza ya kombe la mataifa ya Ulaya iliyopigwa mjini Leipzig.

https://p.dw.com/p/4hDwI
Euro 2024 - Ureno vs Jamhuri ya Czech
Francisco Conceicao (katikati) akishangilia bao wakati wa mechi ya Kundi F kati ya Ureno na Jamhuri ya Czech kwenye mashindano ya soka ya Euro 2024 mjini Leipzig, Ujerumani, Jumanne, Juni 18, 2024.Picha: Sunday Alamba/AP Photo/picture alliance

Jamhuri ya Czech ilionekana kutumia mbinu za kujilinda zaidi na kutegemea mashambulizi ya kushtukiza karibu mchezo wote na mbinu zao zilizaa matunda baada ya Lukas Provod kufunga bao kunako dakika ya 62 ya mchezo.

Hata hivyo bahati haikuwa upande wao baada ya beki Robin Hranac kujifunga mwenyewe kabla ya Conceicao kuwakata maini kwa kufunga bao la dakika za lala salama.

Timu ya taifa ya Ureno, inayotiwa makali na kocha Roberto Martinez ni mojawapo ya timu zinazopigiwa upatu kushinda michuano hiyo japo ushindi huu wa kuungaunga unatilia mashaka uwezo wao wa hatimaye kuchukua ubingwa.

Soma pia: Mbappe avunjika pua katika ushindi wa Ufaransa dhidi ya Austria 

Yote tisa, kumi ni ushindi unaoweka hai matumaini ya nahodha Cristiano Ronaldo kushinda taji lake la pili akiwa na timu yake ya taifa baada ya kulinyakua mnamo mwaka 2016 baada ya kuifunga Ufaransa 1-0 katika mechi ya fainali.

Ureno sasa itavutana mashati na Uturuki mnamo siku ya Jumamosi katika mechi yao ya pili itakayotifua vumbi katika dimba la Signal Iduna Park mjini Dortmund huku Jamhuri ya Czech ikiwa na miadi na Georgia mjini Hamburg.

Euro 2024: Türkei - Georgia
Wachezaji wa Uturuki wakisherehekea bao katika mchezo wao dhidi ya GeorgiaPicha: Julian Stratenschulte/dpa/picture alliance

Kwengineko, kinda wa Real Madrid Arda Guler alionyesha makali yake baada ya kufunga bao maridadi na kuisaidia timu yake ya taifa ya Uturuki kupata ushindi wa 3-1 dhidi ya Georgia, inayoshiriki michuano hiyo ya Ulaya kwa mara ya kwanza katika historia yao.

Soma pia: Waziri wa Uchumi wa Ujerumani asema Michuano ya Euro 2024 ni zawadi kwao

Guler mwenye umri wa miaka 19 na aliyebandikwa jina la utani la "Messi wa Uturuki” ameingia kwenye rekodi kwa kuwa mchezaji wa tatu mwenye umri mdogo zaidi kufunga bao kwenye mechi yake ya kwanza ya michuano ya EURO.

Guler anafuata nyayo za Ferenc Bene wa Ufaransa aliyepachika bao dhidi ya Uhispania mnamo mwaka 1964 na Cristiano Ronaldo aliyefunga bao dhidi ya Ugiriki mnamo mwaka 2004.

Kocha wa Georgia Willy Sagnol ameonesha kuridishwa na wachezaji wake licha ya kampeni yao kuanza kwa kipigo.