COP27: Guterres atoa wito wa kufikia makubaliano
18 Novemba 2022Wapatanishi hao walikabiliana na usiku mrefu wakihangaika kuzuia mazungumzo hayo kuvunjika huku wakitafuta mwafaka kuhusu suala lenye utata la fidia ya hasara na uharibifu vinavyosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa. Mazungumzo hayo ya hali ya hewa yalionekana kukwama hadi usiku wa kuamkia leo hasa katika masuala makubwa ya ufadhili kwa nchi masikini, lakini uwezekano wa makubaliano ulichochewa na pendekezo lisilotarajiwa la Umoja wa Ulaya.
Dakika chache baada ya mwenyekiti wa mkutano huo wa Umoja wa Mataifa wa mazingira Sameh Shoukry, kuwaonya wajumbe kwamba hawajafikia malengo ya kuhitimisha mkutano huo na matokeo thabiti, afisa mkuu wa hali ya hewa wa Umoja wa Ulaya Frans Timmermans, alipendekeza hatua mbili ambazo zingewezesha upatikanaji wa fedha kwa nchi masikini lakini pia kuzishinikiza nchi zote kupunguza kwa kiasi kikubwa uzalishaji wa hewa chafu ya kaboni na hatua kwa hatua kuachana na matumizi ya nishati zote za mafuta, ikiwa ni pamoja na gesi asilia.
Soma zaidi: Guterres:Tuchukue hatua za pamoja ama tuangamie sote
Timmermans amesema ni wazi kuwa mataifa 27 ya Ulaya hayatatoa fedha zaidi kama hakutokuwepo makubaliano juu ya malengo ya uzalishaji wa hewa chafu.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres wakati akirejea nchini Misri kutoka Bali ambako alikuwa amehudhuria mkutano wa viongozi wa G20, ameyatolewa wito mataifa tajiri kufikia makubaliano juu ya msaada wa kifedha kwa nchi zinazoinukia kichumi ili kufidia hasara zinazopata nchi zilizo hatarini zaidi kukumbwa na majanga ya hali ya hewa.
Soma zaidi: COP27: Viongozi kuzungumzia ongezeko la joto duniani
Guterres amesema kumekuwa na uvunjifu dhahiri wa uaminifu kati ya nchi zilizoendelea na zinazoinukia kiuchumi, akiongeza kuwa njia mwafaka zaidi ya kujenga imani itakuwa kupata makubaliano kabambe na ya kuaminika juu ya hasara na uharibifu pamoja na msaada wa kifedha kwa nchi zilizo hatarini huku akisema kuwa huu si wakati wa kunyoosheana vidole:
"Wakati wa kuzungumza juu ya hasara na uharibifu umekwisha. Tunahitaji hatua. Hakuna anayeweza kupinga ukubwa wa hasara na uharibifu tunaoushuhudia duniani kote. Dunia inaungua na kuzama mbele ya macho yetu. Naomba pande zote zionyeshe kuwa zinayaona haya na kuyaelewa. Tumeni ishara ya wazi kwamba sauti za walio mstari wa mbele katika mgogoro huu hatimaye zinasikika. Tutafakari udharura na ukubwa wa changamoto inayozikabili nchi nyingi zinazoendelea. Sasa ni wakati wa mshikamano."
Soma zaidi: Mkutano wa COP27 waanza kwa onyo Misri
Nchi maskini zinakabiliwa na matokeo mabaya ya mabadiliko ya hali ya hewa licha ya kuchangia kwa kiasi kidogo uchafuzi wa mazingira, zimeyashutumu mataifa matajiri zaidi ambayo ndio wachafuzi wakuu wa mazingira kwa kukwamisha makubaliano hayo na kusema hawawezi kusubiri zaidi kabla ya kuundwa kwa fuko la kulipia uharibifu huo.
Mataifa yanayoendelea yametaka kuhakikishiwa katika mkutano huo wa COP27 unaomalizika leo kwamba nchi tajiri hatimaye zitatimiza ahadi ya kutoa dola bilioni 100 kwa mwaka ili kuzisaidia kuinua uchumi wao na kukabiliana na athari za siku zijazo. Mataifa hayo yametoa pia wito wa kufikia makubaliano kabla ya kumalizika kwa mkutano huo.