1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Erdogan ataka ulimwengu usikilize kilio cha Wasyria

17 Novemba 2011

Waziri Mkuu wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, amesema ni lazima sasa dunia isikie mayowe yanayopigwa na Wasyria, huku kundi la Ikhwanul-Muslimina la Syria likisema liko tayari kwa uingiliaji kati wa Uturuki nchini Syria.

https://p.dw.com/p/13CU2
Waziri Mkuu wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan.
Waziri Mkuu wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan.Picha: dapd

Kila dalili inaonesha kwamba Syria sasa inatumbukia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe. Hayo ni kwa mujibu wa Waziri wa Nje wa Urusi, Sergei Lavrov, ambaye ameliambia Shirika la Habari la ITAR-Tass hivi leo (17.11.2011) kuwa ni lazima kwa serikali na wapinzani kuzungumza haraka sana.

Kauli ya Lavrov inafuatia mashambulizi ya hapo jana dhidi ya ofisi ya usalama wa taifa wa Syria, yaliyofanywa na wanajeshi walioasi, na imekuja masaa machache tu baada ya mashambulizi mengine ya hivi leo, dhidi ya ofisi ya vijana wa chama tawala cha Baath.

Lakini ni Waziri Mkuu wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, amekwenda mbali zaidi ya hapo, akitaka pachukuliwe hatua kali kuzuia umwagaji damu nchini Syria.

Akizungumza katika mkutano wa kimataifa wa nishati mjini Istanbul hivi leo, Erdogan ameutaka ulimwengu "kuliangalia suala la Syria kwa hisia kali, kama ulivyoliangalia la Libya, taifa linalozalisha mafuta kwa wingi."

Uturuki ni jirani wa Syria, anayepinga waziwazi operesheni ya utawala wa Rais Assad dhidi ya waandamanaji.

Ikhwanul Muslimina yaunga mkono uingiliaji kati wa Uturuki

Kiongozi kundi la Ikhawanul Muslimina la Syria anayeishi uhamishoni, Muhammad Riadh Shakfa, amesema watu wa Syria wanakubali uingiliaji kati wa Uturuki kuliko wa nchi za Magharibi.

Akizungumza leo katika mkutano na waandishi wa habari mjini Istanbul, Shakfa amesema Wasyria wana haki ya kuomba msada mkubwa kutoka kwa Uturuki, kwa sababu ni majirani zao.

Gazeti linalounga mkono serikali ya Syria, Sabah, limeripoti katka toleo lake la leo, kwamba Baraza la Kitaifa la Syria, ambacho ni chombo kinachowaunganisha wapinzani, limeiomba Uturuki kuweka marufuku ya kuruka ndege kwenye mpaka wake na Syria ili kuwalinda raia.

Haya yanakuja, ikiwa ni siku moja tu baada ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kuisimamisha uwanachama Syria na kuipa muda wa siku tatu kutekeleza mpango wa amani.

Jumuiya ya Nchi za Kiarabu yakaribisha hatua za kimataifa?

Waziri wa Nje wa Qatar, Hamad bin Jasim (kulia) na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi Kiarabu, Nabil al-Arabi Nabil (kushoto).
Waziri wa Nje wa Qatar, Hamad bin Jasim (kulia) na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi Kiarabu, Nabil al-Arabi Nabil (kushoto).Picha: dapd

Wachambuzi wanasema sasa inaonekana Jumuiya hiyo inafungua njia kwa uingiliaji kati kutoka nje, kama ilivyotokea kwa Libya, licha ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar, Hamad bin Jassim Al-Thani, kusema bado nafasi ya kuzuia hilo ipo.

"Hatutaki kusema kwamba hii ni fursa ya mwisho kwa serikali ya Syria, maana sitaki ichukuliwe kama ni onyo. Lakini ninachoweza kusema ni kuwa tunakaribia mwisho wa njia, kwa kiasi ambacho Jumuiya ya Nchi za Kiarabu inaweza kufanya. Tunamuomba Mungu na kutaraji kwamba ndugu zetu kwenye serikali ya Syria watatusaidia, kumaliza maafa haya." Amsema Al-Thani.

Kubadilika kwa maandamano ya amani kuwa mapambano ya silaha, kunatoa fursa zaidi kwa wakosoaji kufikiria uwezekano wa Syria bila ya Assad.

Hata China iliyotumia kura ya veto kuzuia azimio la Baraza la Usalama la Umoja dhidi ya Assad, leo imetoa kauli tafauti. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje, Liu Weimin, amesema China inaweza kufikiria upya ikiwa azimio kama hilo litapelekwa tena.

Ujerumani, Uingereza na Ufaransa, zimesema zitaendelea na kushinikiza kupatikana kwa azimio hilo, hasa baada ya kusitishwa uwanachama wa Syria kwenye Jumuiya ya Nchi za Kiarabu.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AP/AFP/DPA
Mhariri: Josephat Charo