Erdogan awasili Cairo
13 Septemba 2011Erdogan amepokelewa kwa moyo mkunjufu nchini Misri kuanza ziara yenye lengo la kuyaimarisha maslahi ya Uturuki kama rafiki na mshirika wa nchi za kaskazini mwa Afrika.
Kutokana na kuuimarisha umaarufu wake miongoni mwa nchi za Kiarabu, hasa kwa kuchukua msimamo mkali dhidi ya Israel, Waziri Mkuu Erdogan anatarajiwa kusikilizwa kwa makini atakapowahutubia wajumbe kwenye mkutano wa nchi za Kiarabu unaofanyika mjini Cairo.
Erdogan pia atakutana na wawalkilishi wa Baraza la Kijeshi la Misri ambalo sasa linaiongoza Misri kuelekea katika utawala wa kiraia.
Mohammed Adel, mmoja wa wanaharakati mmoja aliyeshiriki katika maandamano ya upinzani dhidi ya utawala wa Rais Hosni Mubarak, amesema ziara hii ya Waziri Mkuu wa Uturki nchini Misri ni muhimu sana. Adel amesema Misri inapaswa kudumisha uhusiano wake na Uturuki.
Akisisitiza umuhimu wa ziara ya Erdogan katika nchi za kaskazini mwa Afrika, mwakilishi mkuu wa wakfu wa Kijerumani wa Friedrich Ebert nchini Uturuki, Michael Meier, amesema kuwa ziara hiyo ina lengo la kuuongeza uzito wa Uturuki katika mataifa hayo.
"Erdogan atahutubia kwenye chuo kikuu cha mjini Cairo na pia atakutana na wawakilishi wa baraza la kijeshi la Misri pamoja na wa jumuiya mbalimbali zilizoshiriki katika harakati za mapinduzi. Hayo yote yana lengo la kuonyesha wazi kwamba Erdogan anadhamiria kujenga mafungamano." Amesema Meier.
Waziri Mkuu huyo wa Uturuki pia anatarajiwa kuwahutubia wajumbe wanaohudhuria mkutano wa Umoja wa Nchi za Kiarabu mjini Cairo. Wajumbe kwenye mkutano huo walikubaliana hapo jana juu ya kukusanya nguvu ili kuwaunga mkono Wapalestina wanaokusudia kuwasilisha maombi kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ili Palestina iweze kutangaza dola yake huru.
Mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Nchi za Kiarabu walikubaliana juu ya msimamo huo kwenye kikao chao kilichohudhuriwa pia na Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Wapalestina, Mahmoud Abbas.
Kikao cha mawaziri hao kilichohudhuriwa pia na Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya, Catherine Ashton. Ashton amesema Umoja wa Ulaya unaunga mkono kufikiwa kwa dola ya Wapalestina kwa njia ya mazungumzo.
Naye akilizungumzia suala la Palestina, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle, anayemaliza zaira ya siku tatu katika Mashariki ya Kati ametahdharisha kwamba njia inayofuatwa na Wapalestina itaziathiri juhudi za amani katika Mashariki ya Kati.
Mwandishi: Abdu Mtullya/AFPE/DRadio Kultur
Mhariri: Josephat Charo