EU yachukua hatua kufuatia mlipuko wa UVIKO-19, China
5 Januari 2023Maambukizi ya UVIKO-19 yameongezeka nchini China hasa katika mji mkuu Beijing. Wanaoathirika zaidi ni wazee. Hospitali ya Chuiyangliu iliyopo mashariki mwa jiji hilo imeshuhudia uhaba wa vitanda vya kuwalaza wagonjwa kutokana na idadi kubwa ya maambukizi.
Ongezeko la wagonjwa mahututi wanaohitaji huduma ya hospitali inajiri baada ya China kuachana mwezi uliopita na hatua yake ya vizuizi vikali vya kukabiliana na janga hili la UVIKO-19, hatua ambazo ziliuelemea uchumi wa taifa hilo na kusababisha maandamano makubwa kuwahi kushuhudiwa tangu mwishoni mwa miaka ya 1980.
Soma zaidi:Ulaya na mkakati wa kuwapima UVIKO-19 abiria kutoka China
Jana, viongozi wa Umoja wa Ulaya waliokutana mjini Brussels nchini Ubelgiji, waliyahimiza mataifa wanachama kuweka kanuni ya kufanywa vipimo vya UVIKO-19 kabla ya safari, kwa abiria wote kutoka China. Hatua hiyo ambayo tayari imekosolewa na mashirika ya ndege, huenda ikaikasirisha Beijing.
Hata hivyo Umoja wa Ulaya haikuafikiana kwamba mataifa yote 27 wanachama yaweke kanuni ya aina hiyo ambayo nchi kama Italia, Ufaransa na Uhispania zilikuwa tayari zinaitekeleza katika ngazi ya kitaifa.
China yapinga hatua hiyo
China tayari imepinga vikali hatua za aina hiyo, ikionya kulipiza kisasi kama sera hiyo itaamuliwa kote katika jumuiya hiyo.
Aidha, Mkuu wa Shirika la Afya Ulimwenguni WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema jana kuwa ana wasiwasi juu ya ukosefu wa data ya mlipuko wa UVIKO-19 kutoka serikali ya China. Shirika hilo limebaini kuwa kufikia Januari 01, 2023, China iliripoti visa vipya vya maambukizi 218,019 na vifo 648.
Soma zaidi: China yakosoa vizuizi vya UVIKO dhidi ya raia wake
Leo Alhamisi, China imesisitiza kwamba imekuwa wazi kwa jamii ya kimataifa juu ya takwimu zake za UVIKO-19 na imetoa wito kwa Shirika la Afya Ulimwenguni kuchukua msimamo "wa haki" juu ya suala hilo.
Wakati huohuo, Wajerumani wanaoishi China wameanza hii leo kupatiwa chanjo ya UVIKO-19 ya BioNTech. Hili ni tukio la kwanza la utoaji wa chanjo ya kigeni katika nchi hiyo ambayo haijaidhinisha matumizi ya chanjo zisizo za Kichina licha ya maambukizi kuongezeka.
Hii ni kutokana na makubaliano yaliyofikiwa mwezi Novemba wakati wa ziara ya Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz mjini Beijing. Wajerumani wenye umri wa miaka 12 na zaidi wanaweza kupokea dozi yao ya kwanza au ya ziada katika hospitali teule ya kimataifa katika miji ya Beijing, Shanghai, Shenyang, Guangzhou au Chengdu.