1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSomalia

EU yasitisha kwa muda ufadhili Somalia

19 Septemba 2023

Umoja wa Ulaya umesitisha kwa muda ufadhili wake kwa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani nchini Somalia, baada ya uchunguzi wa Umoja wa Mataifa kugundua wizi na matumizi mabaya ya misaada.

https://p.dw.com/p/4WXzK
Somalia | Hungerkrise
Watu wanasubiri maji katika kambi, moja ya kambi 500 za wakimbizi wa ndani (IDPs) katika mjiNI Baidoa, Somalia.Picha: Yasuyoshi Chiba/AFP

Kulingana na ripoti ya Julai 7 iliyotajwa kuwa ya "siri kali" iliyoagizwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, ambayo ilichapishwa kwa mara ya kwanza na chombo cha habari kinachofuatilia maendeleo ya kimataifa cha Devex iliwataja wakimbizi wa ndani wadai kwamba walilazimishwa kulipa hadi nusu ya pesa taslimu za msaada walizopata, kwa watu walio katika nafasi za madaraka kwa vitisho vya kufukuzwa, kukamatwa au kufutwa kwenye orodha za wanaostahili kupata misaada.

Soma pia: Mashirika yaunga mkono ombi la UN la dola bilioni 7

Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, Tume ya Ulaya ilitoa msaada wa zaidi ya dola milioni 7 kwa ajili ya operesheni za Shirika la Mpango wa Chakula (WFP)nchini Somalia mwaka jana, ikiwa ni sehemu ndogo ya michango ya zaidi ya dola bilioni 1 iliyopokea.

Hata hivyo msemaji wa Tume ya Ulaya Balazs Ujvari, amesema kwamba kufikia sasa Umoja wa Ulaya haujapewa taarifa na washirika wake Umoja wa Mataifa kuhusu athari za ufadhili wa miradi ya Umoja Ulaya.

Soma pia: Mashirika ya UN yaonya kuhusu njaa kali Somalia

Ujvari ameongezea kwamba wataendelea kufuatilia hali hiyo na kuzingatia mtazamo wao wa kutovumilia ulaghai, ufisadi au utovu wa nidhamu. Lakini Shirika la Mpango wa Chakula Duniani halikutoa tamko lolote kuhusiana na suala hili.

Uchunguzi wa kina

Dürre und Trockenheit am Horn von Afrika
Mwanamke wa Ethiopia akipepeta chakula cha msaada wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani.Picha: Claire Nevill/AP Photo/picture alliance

Kwa mujibu wa afisa mmoja mwandamizi wa Umoja Ulaya aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina uamuzi wa kusitisha msaada kwa muda ulichukuliwa baada ya uchunguzi wa Umoja wa Mataifa kubaini kwamba wamiliki wa ardhi, mamlaka za mitaa, wanachama wa vikosi vya usalama na wafanyakazi wa kibinadamu walikuwa wakishiriki katika kuiba misaada iliyokusudiwa kwa watu walio katika mazingira magumu.

Soma piaUkame Pembe ya Afrika wasababisha njaa kwa watu milioni 13

Afisa huyo alisema kwamba misaada ingerejeshwa baada ya WFP kutimiza masharti ya ziada, kama vile uhakiki wa washirika mashinani nchini Somalia huku chanzo chengine kikisema kwamba tume ya Ulaya inashirikiana kikamilifu na WFP kutatua kasoro za kimfumo lakini hakuna msaada wowote uliositishwa katika hatua hii.

Miezi mitatu iliyopita WFP na Shirika la misaada la Marekani (USAID) walisitisha msaada wa chakula kwa nchi jirani ya Ethiopiakatika kukabiliana na ubadhirifu wa misaada.

Msemaji wa USAID Jessica Jennings alisema katika taarifa yake kwamba Marekani inafanya kazi ili kuelewa ukubwa wa ubadhirifu huo na kwamba iko tayari kuchukua hatua za kuwalinda walengwa na kuhakikisha pesa za walipakodi zinatumika kuwanufaisha watu walio katika mazingira magumu nchini Somalia kama ilivyokusudiwa.