1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EURO 2020: Robo fainali Italia yaibwaga Ubelgiji 2-1

3 Julai 2021

Katika michuano ya kugombea ubingwa wa kombe la Ulaya robo fainali, Italia imeibwaga Ubelgiji 2-1 na Uhispania imeibwaga Uswisi baada ya kuifunga mikwaju ya peneti, mabao matatu kwa moja.

https://p.dw.com/p/3vyFb
EURO 2020 I Italien v Belgien
Picha: Matthias Schrader/AP/picture alliance

Wachezaji wa Uhispania waliweza kutuliza makini na kuweka kimiani mabao hayo matatu ya peneti. Kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2012 Uhispania inaingia nusu fainali katika mashindano ya kugombea ubingwa wa kombe la Ulaya.

Wahispania walianza vizuri na juhudi zao zilileta matunda katika dakika ya nane baada ya mchezaji wa kiungo wa Uswisi, Denis Zakaria kuuchinja mpira na kuuiingiza kwenye goli lake mbele ya mashabiki wa kandanda wapatao 10,000 katika mji wa Urusi wa St Petersberg.

Timu ya Uhispania katika michuano ya EURO 2020
Timu ya Uhispania katika michuano ya EURO 2020Picha: Kirill Kudryavtsev/REUTERS

Timu ya Uswisi iliyomng'oa bingwa wa dunia Ufaransa kwa mikwaju ya peneti ilipatikana na mkosi mwingine baada ya mshambuliaji wao hatari Breel Embolo kuumia na kushindwa kuendelea kulisakata soka. Hata hivyo timu ya Uswisi ilirejea na nguvu mpya katika nusu ya pili ya mchezo na kuibana Uhispania. Zakaria alikosakosa goli la kusawizisha katika dakika ya 56. Hakika angeliweza kufuta machozi laiti kichwa alichopiga kingelijaa kimeani.

Uswisi hatimaye ilipata goli la kusawazisha lililofungwa na mshambuliaji Xherdan Shaqiri katika dakika ya 68 lakini juhudi za wachezaji wa Uswisi zilianza kuvunjika baada ya mchezaji wao hodari wa kutoa pasi, Freuler kuonyeshwa kadi nyekundu kutokana na kucheza rafu.

Kwa jumla timu ya Uswisi inastahili pongezi kwa kufanikiwa kufika hadi robo fainali kwa mara ya kwanza katika mashindano ya kugombea kombe la ubingwa wa Ulaya licha ya kutolewa timu hiyo imeweka historia ya kandanda barani Ulaya.  

Mbele: Mchezaji Xherdan Shaqiri na wenzake wa timu ya Uswisi
Mbele: Mchezaji Xherdan Shaqiri na wenzake wa timu ya UswisiPicha: Dmitri Lovetsky/Getty Images

Kwingineko Ubelgiji na Italia zilijikita katika robo fainali ya pili kwenye uwanja wa mjini Munich kwenye jimbo la Bavaria la kusini mwa Ujerumani. Italia imeondoka na ushindi wa mabao mawili kwa moja. Sasa wanajinoa kupambana na Uhispania. Mechi ya timu hizo mbili haukuwa ya  tamasha la magoli lakini mchezo ulikuwa mkali na wa kusisimua sana.

Mpaka sasa Italia imethibitisha kuwa timu bora kwenye mashindano, wakati timu ya Ubelgiji  iliwekewa matumaini ya juu kutokana na uhodari wa kila mchezaji binafsi. Mabao mawili ya Italia yalikuwa ya ufundi mkubwa. Nicolo Barella wa Italia alifungua dimba kwa kuzititikisa nyavu za goli la Ubelgiji. Alifuatiwa na Lorenzo Insigne aliyekamilisha kazi kwa kuipatia timu yake bao la pili.

Romelu Lukaku kwenye mpambano na timu ya Italia EURO 2020
Romelu Lukaku kwenye mpambano na timu ya Italia EURO 2020Picha: Matthias Hangst/AFP/Getty Images

Ubelgiji ilipata matumaini kidogo katika dakika za mwisho za nusu ya kwanza baada ya mchazaji wa Italia Giovanni di Lorenzo kumchezea rafu Jeremy Doku wa Ubelgiji. Mshambuliaji hatari ya Ubelgiji Romelu Lukaku alipiga peneti la kuujaza mpira wavuni. Wabelgiji waliongeza kasi lakini hawakufanikiwa kuipenya ngome ya Italia hadi kipenga cha mwisho kilipopulizwa. Italia sasa itapambana na Uhispania kwenye uwanja wa Wembley jumanne ijayo.

Katika robo fainali za pili leo Jumamosi England itamenyana na Ukraine kwenye uwanja wa Olimpico wa mjini Rome, Italia wakati timu ya Jamhuri ya Czech itachuana na Denmark.

EURO 2020 Raheem Sterling na timu yake ya Uingereza
EURO 2020 Raheem Sterling na timu yake ya UingerezaPicha: Catherine Ivill/REUTERS

Wakati huo huo waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Horst Seehofer ambaye hapo awali alikuwa mwenyekiti wa chama cha CSU katika jimbo la Bavaria hakuchelewa kukumbusha juu ya hatari ya maambukizi ya virusi vya corona kutokana na mikusanyiko ya watu wengi kwenye viwanja vya mpira. Amelilaumu shirikisho  la vyama vya kandanda la bara la Ulaya kwa kushikilia kuruhusu idadi kubwa ya mashabiki wa kandanda kuingia viwanjani. Amesema sera hiyo si ya uwajibikaji.

Vyanzo:/AFP/RTRE