EURO 2024: France yalazimishwa sare ya 0-0 na Netherlands
24 Juni 2024Nahodha msaidizi wa Ufaransa, Antoine Griezman alishindwa kuzitumia vyema nafasi za wazi wazi, huku bao la Xavi Simons wa Uholanzi nalo likikataliwa na kuifanya mechi hiyo kuwa ya kwanza kumalizika bila ya kufungana tangu michuano hii ilipoanza.
Matokeo haya yanazifanya timu hizo mbili kubakia na pointi nne kila moja katika kundi D baada ya mechi za mzunguko wa pili. Poland ndio itaanza kuyaaga mashindano hayo kwenye kundi hili baada ya kufungwa mabao 3-1 na Austria katika mechi ya jana jioni na kuendelea kushika mkia. Na hata kama itaifunga Ufaransa katika mechi ya mwisho ya hatua ya makundi, bado haitakuwa na nafasi ya kusonga mbele.
Soma pia: Ujerumani yawa ya kwanza kufuzu duru ya mtoano
Uholanzi itakwaana na kisiki Austria ambao wameonyesha mchezo mzuri katika mechi zake za awali.
Minong'ono ilihanikiza kabla ya kuanza kwa mechi hiyo, ikiwa Mbappe atacheza na hasa kutokana na majeraha ya pua aliyoyapata kwenye mechi iliyopita ya ufunguzi dhidi ya Austria, ambapo Ufaransa iliibuka na ushindi wa bao 1-0.
Mbappe siku ya Alhamisi alionekana mazoezini akiwa amevaa barakoa na kocha wa Ufaransa Didier Dechamps alikuwa na matumaini kwamba angeweza kucheza. Lakini Dechamps baadae alisema haoni sababu ya kumtia hatarini Mbappe kwa kumchezesha kwenye mechi ambayo hawakulazimika sana kushinda.
Ufaransa, ilikosa nafasi kama tatu za wazi katika kipindi cha pili, baada ya Aurélien Tchouaméni, Griezmann na Ousmane Dembele kushindwa kupenya kwenye lango la Uholanzi lililodhibitiwa na Bart Verbruggen.
Katika dakika ya 69, Xavi alipiga shuti maridadi lililompita kipa wa Ufaransa Mike Maignan, ingawa hata hivyo goli hilo lilikataliwa baada ya kubainika kwamba Denzel Dumfries alikuwa ameotea na kumzuia Maignan kuokoa shuti hilo la Xavi.
Griezman amekiri baada ya mechi hiyo kwamba alikuwa na nafasi nzuri za kuifungia timu yake na kusema ilikuwa ni aibu kubwa kushindwa kufunga licha ya kuwa na mpira tena karibu na goli. Amesema walikuwa imara katika safu ya ulinzi na hata kimbinu, lakini walichoshindwa ni kufunga goli.
Soma pia: Ufaransa yaisambaratisha Uholanzi 4-0
Mbappe naye anakiri kwamba Ufaransa ilishindwa kutumia nafasi walizopata na kusema kuwa cha msingi kwao kwa sasa ni kuhakikisha wanacheza vizuri zaidi ili kushinda. Naye amekiri kwamba walitengeneza nafasi nzuri lakini walishindwa kuzitumia ili kuondoka na ushindi. Mbappe akasema kuna namna wanahitaji kujirekebisha.
Kwa upande wa Uholanzi ni kilio kitupu. Nahodha wake Virgil van Djik alilalama kamba walinyimwa bao lililofungwa na Xavi. Akasema Ufaransa walikuwa na nafasi zao, na wao pia walikuwa na nafasi moja ama mbili za kufunga.
Mashabiki wa Uholanzi walifurika pomoni kwenye uwanja wa Leipzig na mji wa Leipzig ulifunikwa na rangi ya chungwa kabla ya mechi hiyo. Licha ya mashabiki wa Ufaransa kujitutumua, lakini hawakufua dafu. Inasemekana mmoja ya mashabiki wa Ufaransa alikwenda na jogoo uwanjani hapo usiku wa kuamkia siku ya mechi. Haikuwa wazi ikiwa jogoo huyo naye alikua na tiketi ya kutazama mechi.
Kwenye mechi ya awali ya kundi D, Austria ilishinda mabao 3-1 dhidi ya Poland ambayo kimsingi tayari imeyaaga mashindano hayo ya Euro 2024, licha ya kumchezesha nahodha wake Robert Lewandowski.