1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

G7 yaonya dhidi ya kuubadilisha mfumo wa kimataifa kwa nguvu

17 Aprili 2023

Kundi la nchi saba zinazoongoza kwa uchumi wa viwanda duniani, G7, limeonya dhidi ya hatua yoyote ya kujaribu kubadilisha mfumo wa kimataifa unaotawaliwa na mataifa ya Magharibi kutokana na vita vya Urusi nchini Ukraine

https://p.dw.com/p/4QBgl
Japan G7 Gipfel Treffen der G7-Außenminister
Picha: Andrew Harnik/REUTERS

Waziri wa mambo ya kigeni wa Japan, Yoshimasa Hayashi, amesema watapinga kwa nguvu zote jaribio lolote la upande mmoja la kubadilisha mfumo wa kilimwengu kwa kutumia nguvu. Ameyasema hayo hii leo asubuhi wakati yeye na mawaziri wenzake wa kundi la G7 wakijadili hali katika eneo la Indo Pasifiki katika mkutano wao unaofanyika nchini Japan.

Yoshimasa Hayashi ameongeza kwamba wako tayari kuionesha dunia kuwa wana nia thabiti ya kuheshimu utaratibu wa kimataifa unaozingatia utawala wa sheria. Kulingana na taarifa iliyotolewa na wizara ya kigeni ya Japan, baada ya kikao cha kwanza cha mawaziri hao wa G7, kundi hilo linaendelea na msimamo wa kuiwekea vikwazo Urusi kufuatia uvamizi wake nchini Ukraine pamoja na kupinga tangazo la rais Vladimir Putin wa Urusi la kutuma silaha za nyuklia nchini Belarus.

Mawaziri wa G7 waahidi kuachana na mafuta ya visukuku

Hayashi ameongeza kwamba ni muhimu kundi hilo kuungana kwa sauti moja na kuendelea kutoa misaada kwa Ukraine pamoja na kuliunga mkono taifa hilo. Mkutano huo ulikubaliana kwamba Urusi ni lazima iwaondoe wanajeshi wake wote, silaha na magari ya kivita nchini Ukraine haraka iwezekanavyo bila masharti yoyote.

Uchokozi wa China unaokua na mzozo wa Sudan pia zitajadiliwa katika mkutano wa G7

Konflikte im Sudan
Mkuu wa utawala wa kijeshi Sudan, Abdel Fattah al-BurhanPicha: Marwan Ali/AP/dpa/picture alliance

Kingine ambacho kimwekwekwa katika ajenda ya kujadiliwa katika mkutano huo ni uchokozi wa China kwa Taiwan pamoja na hatua ya Korea Kaskazini kufanya majaribio ya makombora ya masafa marefu. Vurugu za hivi karubuni zinazoendelea nchini Sudan pia zitajadiliwa katika mkutano huo.

Jana Jumapili mawaziri hao walijadili kwa zaidi ya masaa mawili changamoto zilizoko katika eneo la Indo Pasifiki, ikiwemo vitisho vya china na Korea Kaskazini. Hayashi alielezea wasiwasi wake juu ya kitisho cha majini cha China katika bahari ya Mashariki na Kusini mwa China, pamoja na kuzungumzia pia hatua ya hivi karibuni  ya raia wa Japan kukamatwa na serikali ya China. Hayashi ameshauri kuwa ni muhimu kuitolea mwito China kufaya vitendo vyake kama mwanachama aliyewajibika katika Jumuiya ya Kimataifa.

Mawaziri wa kigeni wa G7 kujadili usalama wa Ulaya na kanda ya bahari ya Hindi na Pasifik katika mkutano wao

Mkutano huo wa G7 unafanyika kuelekea mkutano wa kilele wa marais wa kundi hilo unaotarajiwa kufanyika mjini Hiroshima Japan mwezi Ujao. Japan kwa sasa ndio inayoshikilia urais wa kupokezana wa kundi hilo linalozijumuisha Uingereza, Canada, Ujerumani, Italia na Marekani.

Chanzo: reuters, dpa