Ghana yathibitisha maambukizo ya kwanza ya mpox
4 Oktoba 2024Mamlaka za nchi hiyo zimesema mgonjwa aliyegundulika ni kijana kutoka mkoa wa Kaskazni Magharibi ulio kiasi umbali wa kilometa 475 kutoka mji mkuu Accra.
Mkuu wa huduma za afya nchini humo Patrick Aboagye amesema kijana huyo alionesha dalili za malengelenge mwilini, homa na maumivu ya viungo.
Soma zaidi: Rwanda yaanza chanjo ya Mpox
Tayari ameruhusiwa lakini maafisa wa afya wanawafuatilia watu wengine 25 ambao inaaminika walikutana na mgonjwa huyo.
Wakati hayo yakiarifiwa, Shirika la Afya Duniani (WHO) limeidhinisha leo Ijumaa kipimo cha kwanza cha ugonjwa wa mpox, hatua ambayo itayasaidia mataifa duniani yanayopambana kudhibiti maradhi hayo hatari.
Taarifa ya WHO iliyotolewa leo imesema ithabiti ya kutumika kipimo hicho kwa dharura ni muhimu katika kuongeza uwezo wa kubaini maambukizi kwenye mataifa yaliyokumbwa na mlipuko wa ugonjwa wa mpox.
Zaidi ya watu 800 wamekufa barani Afrika kutokana na ugonjwa wa mpox na tayari mataifa 16 yamethibitisha kugunduliwa visa vya maradhi hayo.