Guterres aomba kikosi kipelekwe Haiti kuzima uhalifu
10 Oktoba 2022Katika barua yake kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Katibu Mkuu Guterres amezitaka nchi wanachama wa baraza hilo kupeleka haraka kikosi cha kuingilia kati katika nchi hiyo ya Karibeani, kudhibiti alichokitaja kuwa ''hali ya ghasia inayokithiri.''
Soma zaidi: Hali ni ya kukata tamaa Haiti, UN yaambiwa
Barua yake hiyo imefuatia tamko la Haiti kuwa imeomba rasmi msaada wa kimataifa, kutuliza hali mbaya ya usalama ambayo imelizidi uwezo jeshi lake la polisi. Haiti, nchi maskini zaidi kwenye ukanda wa Amerika, inajikuta katika mzozo mpana wa kisiasa, kiuchumi, kiusalama na kiafya, ambao umelemaza mfumo wa utawala wa sheria.
Kipindupindu katika mitaa ya mabanda
Tangu Alhamisi iliyopita, Umoja wa Mataifa umekuwa ukitoa tahadhari juu ya uwezekano wa mripuko mkubwa wa ugonjwa wa kipindupindu nchini humo, kufuatia kutangazwa kwa visa kadhaa vya ugonjwa huo, vya kwanza katika muda wa miaka mitatu, ikiwa pamoja na vifo visivyopungua saba.
Daktari Nadege Sainvilus anayefanya kazi na shirika la madaktari wasio na mipaka katika makaazi ya mabanda ya Cité Soleil kwenye mji mkuu wa Haiti, Port-au-Prince amesema ''mwanzoni mwa wiki tulipokea visa zaidi ya 20 vya maambukizi ya ugonjwa wa kipindupindu, na kwa bahati mbaya, Jumatano iliyopita, wagonjwa wawili walipoteza maisha.''
Soma zaidi: Mkuu wa haki za binadamu wa UN Bachelet alaani machafuko ya magenge Haiti
Hata hivyo amefurahi kwa tangu hapo hawajasajili kifo kingine katika kituo chao, ambako zaidi ya watu mia moja wamelazwa hospitalini.
Ni lazima kurejesha uthabiti wa Haiti
Katika barua yake kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, katibu mkuu wa umoja huo amesititiza ulazima wa kurejeshwa kwa usalama nchini Haiti, ili kuweza kulinda huduma za mahitaji muhimu, miundombinu ya usafiri na mafuta, na kuyakabili magenge ya wahalifu.
Antonio Guterres amesema ni lazima kuyatilia maanani malengo hayo ili kuuvunja mzunguko wa ghasia katika nchi hiyo na kuirejeshea uthabiti.
Tangu katikati mwa mwezi Septemba, kituo kikuu cha kuingizia mafuta yanayoagizwa kutoka nje cha Varreux kinadhibitiwa na magenge ya wahalifu yaliyojihami kwa silaha.
Soma zaidi: Mkuu wa genge Haiti atishia kuwaua mateka wamishonari
Katika barua yake ya Jumapili Katibu Mkuu Antonio Guterres ametilia mkazo hali katika kituo hicho, akisema inatatiza juhudi za kupambana na mripuko wa kipindupindu, kwa kuzuia uingizaji wa mahitaji muhimu kama maji safi ya kunywa.
Vyanzo: afpe, ape