Guterres: Ulimwengu ni lazima uiokoe Lebanon
24 Septemba 2024Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesema katika ufunguzi wa mkutano wa 79 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Jumanne, Septemba 24, 2024 mjini New York kwamba watu wa Lebanon, watu wa Israel na ulimwengu mzima ni lazima wahakikishe kuwa Lebanon haigeuki na kuwa Gaza nyingine.
Soma: Iran yaelezea wasiwasi kuhusu makabiliano ya Israel na Hezbollah
Guterres ameeleza wasiwasi wake kutokana na mapigano yanayoongezeka katika eneo linalozitenganisha Israel na Lebanon na idadi kubwa ya raia wanaopoteza Maisha na wanaojeruhiwa wakiwemo watoto na wanawake. Guterres ametoa mwito wa kufanyika mageuzi kwenye Umoja wa Mataifa.
Guterres amesema :- "Ninatoa wito kwenye mkutano huu wa kilele wa kuzingatia mageuzi ya kina, ili kuzifanya taasisi za kimataifa kuwa mfano wa kusimamia haki na ufanisi kulingana na maadili ya Umoja wa Mataifa. Kwa sababu ulimwengu wetu unaelekea kwenye njia panda, tunahitaji kufanya maamuzi magumu ili kurejea kwenye mstari."
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesema kutokujali, kutokuwepo na wa usawa na kutokuwa na uhakika ni mambo yanayotengeneza ulimwengu usio endelevu ambapo baadhi ya nchi zinaamini kwamba haziwezi kupewa adhabu yoyote na pia zinapaswa kuogopwa. Amesema haiwezekani dunia kuendelea hivi.
Rais wa Brazil Lula Inacio Da Silva ambaye pia ametoa hotuba yake jioni hii, katika mkutano huo, pamoja na mengine amesikitishwa na hatua ya kutengwa kwa kanda ya Amerika Kusini na bara la Afrika katika baraza la usalama.
Rais wa Marekani Joe Biden ametoa hotuba yake ya mwisho kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa hii leo Jumanne huku mataifa yakiwa yamegawika kutokana na vita kwenye Ukanda wa Gaza, Ukraine na Sudan na pia kitisho cha kuzuka mzozo mkubwa katika eneo la Mashariki ya Kati.
Soma: Israel yafanya shambulizi jipya Lebanon baada ya mauaji ya watu 492
Biden alitumia hotuba yake hiyo amezungumzia haja ya kumaliza mzozo wa Mashariki ya Kati na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miezi 17 nchini Sudan na pia amesisitiza uungaji mkono wa Marekani na Washirika wake wa Magharibi kwa serikali ya Ukraine tangu Urusi ilipoivamia nchi hiyo mwezi Februari mwaka 2022.
Kiongozi huyo wa Marekani ametumia fursa hiyo kusisitiza misaada thabiti kwa Ukraine. Misaada hiyo inaweza kukatishwa ikiwa Rais zamani Donald Trump, ambaye analaumu na kupinga gharama ya vita vya Ukraine, atamshinda Makamu wa Rais Kamala Harris katika uchaguzi wa mwezi Novemba.
Leo hii Jumanne, wawakilishi wa Uturuki, Jordan, Qatar, Iran na Algeria wanatazamiwa kupanda jukwaani kushinikiza hatua za kusitishwa mapigano katika Ukanda wa Gaza.
Ukraine pia imo katika ajenda ya leo Jumanne. Rais Volodymyr Zelensky anatarajiwa kuzungumzia kuhusu vita vya Urusi dhidi ya nchi yake Ukraine.
Hata hivyo haijulikani kama mkutano huo wa kidiplomasia wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa unaweza kufikia lolote litakaloweza kuwapa afueni mamilioni ya watu walio katika migogoro na umaskini duniani kote.
Viongozi wa dunia wanashiriki kwenye mkutano huo wa kila mwaka wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa wakati ambapo Israel na wanamgambo wa Hezbollah nchini Lebanon wanaelekea kutumbukia kwenye vita vikubwa na wakati huo huo vita vya Israel dhidi ya Hamas katika Ukanda wa Gaza vinavyokaribia mwaka mmoja vinazidi kumwaga damu.
Jumuiya ya kimataifa imepaza sauti juu ya kuongezeka kwa ghasia kati ya Lebanon na Israel, na imetahadharisha kwamba kuna uwezekano wa mgogoro huo kutanuka na kuwa wa kikanda.
Vyanzo: DPA/AFP/AP