Haiti yaunda baraza la mpito la uchaguzi wa mwaka 2026
19 Septemba 2024Ofisi ya Waziri mkuu imesema baraza hilo la mpito lililoundwa jana tayari lina viti saba vinavyowakilisha makundi ya kidini, waandishi wa habari, wakulima na vyama vya wafanyikazi.Hata hivyo viti vyengine viwili – kimoja cha mashirika ya haki za binadamu na kingine kwa ajili ya makundi ya wanawake, bado havina mwakilishi. Nchi hiyo yaCaribbean ilifanya uchaguzi mkuu mara ya mwisho mnamo mwaka 2016. Kwa kawaida, uchaguzi unafaa kufanyika kila baada ya miaka mitano lakini kutokana na hali ya kisiasa kuwa tete na kufuatia ombwe la madaraka lililosababishwa na kuuawa kwa Rais Jovenel Moise mwaka 2021, tangu wakati huo nchi hiyo imekuwa bila rais. Makundi yenye silaha yametanua udhibiti wao na sasa yanatawala takriban asilimia 80 ya mji mkuu wa Port-au-Prince na maeneo mengine ya taifa hilo.