Hali yatulia: Afrika Kusini yakwepa kumkamata Putin
22 Julai 2023Mtanziko wa sera ya kigeni wa Afrika Kusini umetoweka - Rais wa Urusi Vladimir Putin hatasafiri kwenda kwenye mkutano wa kilele wa BRICS mjini Johannesburg mnamo Agosti. Hii sio tu inamaliza uvumi juu ya matokeo yanayoweza kutokea ikiwa rais wa Urusi angekanyaga ardhi ya Afrika Kusini. Ajenda ya mkutano wa wakuu watano wa nchi na serikali za nchi washiriki za Brazil, India, China, Afrika Kusini na Urusi pia inaweza kujadiliwa bila kipingamizi - na Putin pengine atakuwa huko kupitia kiunga cha video.
Usihatarishe vita na Urusi
Kama mbadala, Putin anamtuma Waziri wa Mambo ya Nje Sergei Lavrov kwenda Afrika Kusini, ambayo kwa hivyo imeachiliwa kutoka kwenye mtanziko wa kisiasa: kutekeleza hati ya kukamatwa ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu iliyoko The Hague, ICC, dhidi ya Putin atakapowasili. Afrika Kusini ilitia saini Mkataba wa Roma ambao chini yake ICC ilianza kazi yake mwaka 2002. Mahakama hiyo ya jinai, ambayo inashughulikia uhalifu dhidi ya ubinadamu, iliomba kukamatwa kwa Putin mwezi Machi kwa madai kwamba Urusi iliwahamisha watoto wa Ukraine isivyo halali.
Soma pia: Algeria yatuma maombi kujiunga na kundi la BRICS
Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa alikuwa amejitokeza kwa muda mrefu, akiiomba ruhusa ICC kwa misingi kwamba kumkamata Putin kunaweza "kuhatarisha usalama, amani na utulivu wa nchi": Kutekeleza amri ya ukamataji kunaweza kuhatarisha "usalama, amani na utulivu wa nchi". "Itakuwa kinyume na katiba yetu kuhatarisha vita na Urusi," Ramaphosa alisema katika taarifa ya maandishi kwa mahakama. Hata hivyo, Afrika Kusini pia ni mshirika wa karibu wa Urusi.
Afrika Kusini chini ya shinikizo
Afrika Kusini ingekuwa katika hali ngumu sana, anasema mchambuzi Daniel Silke wa mjini Cape Town. "Kungekuwa na uwezekano wa kutii amri ya ukamataji ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, na hilo lingeiaibisha Afrika Kusini," Silke anasema katika mahojiano ya DW. "Kwa kuzingatia ukweli kwamba kuna uhusiano mkubwa kati ya nchi hizo mbili, iliamuliwa kutoka upande wa Urusi kutoutia doa uhusiano ambao ni muhimu kwa Moscow."
Uhusiano umekua zaidi katika miongo kadhaa iliyopita: Umoja wa Kisovieti umekiunga mkono chama cha African National Congress, ANC, cha Afrika Kusini katika mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi. Katika vita dhidi ya Ukraine, Afrika Kusini inajitaja rasmi kuwa isiyoegemea upande wowote, na inafanya majaribio ya upatanishi ili kupata suluhu ya amani ya mzozo huo. Lakini sasa chama kikubwa zaidi cha upinzani, Democratic Alliance, DA, kiliweka shinikizo kwa serikali. DA ilikuwa imehimiza kufuata mikataba ya kimataifa na kukamatwa kwa Putin mara tu atakapowasili.
Hata hivyo, kulingana na Silke, haikuwa rahisi kwamba Putin angetembelea Afrika Kusini katika tukio la mkutano wa kilele wa BRICS mjini Johannesburg kuanzia tarehe 22 hadi 24 Agosti. Mkutano huo wa kilele wa mataifa yenye uchumi unaoinukia ungegubikwa na uwepo wa Putin na uwezekano wa kukamatwa kwake na hivyo kuvurugwa katika ajenda yake kuu, Silke anasema. Hiyo ni kutafuta njia ya kuunda aina fulani ya usawa au kupingana na ushawishi wa Magharibi.
"Na hivyo ndivyo Urusi na China zinataka," Silke alisema. Huo ndio ulikuwa "ufunguo" wa kukubaliana kwamba Putin hangesafiri. Lakini bila shaka, shinikizo la kimataifa, hasa uamuzi wa Mahakama ya Uhalifu, umemzuia Putin kwenda zaidi ya Moscow: "Umezuia uhuru wake wa kutembea, na bila shaka hii itazuia uhuru wake wa kutembea katika sehemu nyingine nyingi za dunia," Silke anaiambia DW.
Somam pia: Rais wa Afrika Kusini awasili Urusi kama sehemu ya ujumbe wa amani
Mwanauchumi wa kisiasa Ronak Golpaldas ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba matokeo hayo yanairuhusu serikali ya Ramaphosa kudumisha msimamo wake kama serikali inayoheshimu utawala wa sheria.
Ghadhabu za Magharibi zaepukwa
Alisema sheria iko wazi juu ya wajibu wa Afrika Kusini ndani na nje ya nchi. "Walipaswa kumkamata Putin baada ya kuwasili. Na kama hili lisingetokea, Pretoria ingekuwa katika matatizo makubwa - sio tu katika suala la utawala wa sheria, lakini pia katika mtazamo wa jumuiya ya wafanyabiashara na jumuiya ya kimataifa," anasema Golpaldas.
Athari kwenye masoko ya fedha zingekuwa kubwa. Randi ya Afrika Kusini tayari imedhoofika kwa kiasi kikubwa kutokana na uchumi unaosuasua na mzozo mkubwa wa nishati nchini Afrika Kusini.
Doudou Sidibé, profesa wa uhusiano wa kimataifa katika Chuo Kikuu cha Gustave Eiffel mjini Paris, pia alikuwa na hofu kwamba ikiwa Afrika Kusini haitamkamata Putin, "itasababisha ghadhabu au ukosoaji wa nchi za Magharibi". Afrika Kusini ingetajwa kama nchi ambayo inakiuka kanuni za kimataifa, Sidibé alisema. Mazungumzo na Putin yalituliza hali kwa rais wa Afrika Kusini na upinzani.